Tembo wasababisha kilio kwa wakulima Kasulu

NA RESPICE SWETU

KUNDI la tembo wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 20, wamevamia mashamba ya wakulima katika Kijiji cha Kagerankanda kilichopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na kuharibu zaidi ya ekari 10 za mahindi na mazao mengine.
Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Omary Mohammed (mwenye shati la kijani) akishuhudia uharibifu uliofanywa na tembo hao akiwa na wakulima walioathirika pamoja na wananchi wengine.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka katika kijiji hicho, Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu,Mohamed Omari amesema kuwa, wamekwenda kwenye kijiji hicho kushuhudia uharibifu huo ikiwa ni pamoja kuwaondoa tembo hao kwenye mashamba ya wakulima.

Ameeleza kuwa, Ili kuwaondoa tembo hao, walilazimika kupiga risasi hewani huku wakichukua tahadhari za usalama wao kwa kuzingatia uelekeo wa upepo wakati wa tukio.

"Tumetumia bunduki aina ya short gun na kupima risasi kadhaa hewani kuwaondoa kwenye mashamba hayo tukiwa tunakinzana na uelekeo wa upepo katika kujilinda na wanyama hao ambao hutegemea uelekeo wa upepo kutambua walipo maadui zao,"alisema.

Kutokana na uharibifu uliofanyika, taratibu za malipo ya fidia kwa wahanga hao zimeanza ambapo hatua ya kwanza ni kujaza fomu maalumu zitakazopelekwa kwenya wizara ya maliasili na utalii kwa ajili ya mchakato wa kulipa fidia .

Omary amefafanua kuwa, taratibu za ulipaji wa fidia zitokanazo na uharibifu wa wanyamapori zipo kwenye sheria namba 5 ya wanyamapori ya mwaka 2009 inayoruhusu malipo ya fidia hizo kwa mazao yaliyoharibiwa na wanyamapori pale tu mazao hayo hayamo kwenye eneo lililozuiliwa au karibu na vyanzo vya maji.

"Mashamba hayo hayakuwa ndani ya eneo la hifadhi wala jirani na chanjo cha maji, hivyo wakulima hao wamepewa fomu za kujaza Ili kuendelea na mchakato wa kudai fidia zao,"amesema.

Omary amewataja wakulima ambao kundi la tembo liliingia kwenye mashamba yao na kufanya uharibifu huo kuwa ni Nkwabi Kadogosa na Hamisi Bujenja huku jina la mkulima wa tatu likiwa bado halijafahamika.

Tukio hilo linafuatia tukio la hivi karibuni ambapo mnyama aina ya kiboko alisababisha uharibifu wa mazao na kuhatarisha maisha ya wakazi wa kijiji cha Rungwempya mapema mwaka huu ambapo pamoja na jitihada za kumsaka zilizofanywa na ofisi ya wanyamapori kwa kushirikiana na wananchi, hajapatikana mpaka leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news