Vyombo huru vya habari ni chachu ya maendeleo katika jamii na Taifa

NA DIRAMAKINI

IMEBAINISHWA kuwa, vyombo huru vya habari ni msingi shirikishi wa kuchakata na kusambaza fikra mpya kwa kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kupitia nyanja mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph katika mahojiano na DIRAMAKINI wakati akizungumzia kuhusu umuhimu wa kuwa na vyombo huru vya habari ambavyo vitawajibika kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla nchini.

Picha na mindecology.

"Kwa hiyo, vyombo huru vya habari ni msingi wa mambo yote, kukosekana kwa vyombo huru vya habari, ni vigumu Serikali haitapata maendeleo, kwani maendeleo ni pamoja na fikra mpya, fikra chanya za kuweza kujenga na ndio maana hata Mwenyezi Mungu alianza na neno yaani neno ni chanzo cha uumbaji wa kila kitu, ndio chanzo cha maendeleo.

"Kama binadamu hatatoa neno, hatasema, hatatamka au kuongea maana yake hapo umefunga hakuna uhai na maendeleo katika taifa yatakosekana kwa kiwango stahiki.

"Maana yake watu wakiwa kimya, huwezi kujua kinachoendelea, lakini Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) anataka sheria zifumuliwe, zitengenezwe zisiwe kandamizi kwa sababu kama utaendelea kubinya hizo sheria mwisho wa siku nchi kama nchi inaweza ikapoteza amani, ukifuatilia katika maeneo mengi duniani, nchi nyingi ambazo amani zimetoweka unaweza kuona kwa kiwango kikubwa, chanzo ni pamoja na mbinyo wa mawazo,"amesema Mwalimu Makuru.

Mwalimu Makuru ameyasema hayo ikiwa, tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka juzi katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Makuru ameendelea kufafanua kuwa, "Lakini pia mbinyo wa mawazo unapokuwepo kinachofuata hapo ni chuki, pia uwajibikaji wa viongozi unakosekana.

"Chanzo cha mataifa mengi kuingia katika mivutano ya wenyewe kwa wenyewe ni pamoja na mbinyo wa demokrasia, na uhuru wa vyombo vya habari au uhuru wa mtu mmoja mmoja kujieleza.

"Sasa ili amani iendelee kustawi nchini,Mheshimiwa Rais Dkt.Samia akagundua ili kuendelea tunu amani lazima uachie uhuru wa vyombo vya habari, watu wajieleze kwa uhuru, mikutano ya vyama vya siasa iwepo sio kwamba watu walitaka kuna watu hawakutaka, lakini amechia watu wawe huru.

"Watu washikamane, wawe wamoja, lakini pia Rais amegundua akiacha uhuru wa vyombo vya habari uwepo utamsaidia yeye kufanya kazi kwa kubaini maovu.

"Nikupe mfano hivi majuzi imerushwa video fupi,mwalimu anamuadhibu mtoto vikali, kutokana na umuhimu wa vyombo vya habari, video ile ilisambaa kwa kasi na mamlaka husika zikachukua hatua,hivyo vyombo huru vya habari vina nafasi na mchango mkubwa sana katika kulijenga Taifa letu,"amefafanua Mwalimu Makuru.

Kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amebainisha kuwa,Rais Dkt.Samia anachokitaka chochote kinachofanyika watu wakione na watu waweze kusema kama kuna uzuri au ubaya ili mradi tu mambo yote yawe ya kweli.

"Lakini kimsaidie yeye Mheshimiwa Rais kufahamu na kung'amua wapi panavuja, kiongozi gani hawajibiki, lengo ni kumsaidia pia maendeleo yazidi kupatikana kwa upana wake nchini. Lakini vyombo vya habari kama vimeminywa, uhuru wa kuongea na kujieleza umebinywa ni shida kwa hiyo Rais anachokitaka ni ufanisi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ufanisi huo unakuja pamoja na watu kutoa mawazo yao kwa uhuru na pia kuwapa uhuru wananchi wa kujieleza na kutoa maoni pasipo kubanwa.

"Mataifa mengi ya Ulaya yameendelea kwa sababu ya freedom of speech, huwezi na hapawezi kuwepo na uhuru wa kujieleza kama umebinya sheria.

"Sheria ndizo zinawapa watu uhuru kamili wa kujieleza. Sasa ili maendeleo yazidi kuonekana na kutekelezeka watu lazima wawe huru. Sasa tukitaka turudi kwenye Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ndani ya sheria ile kuna vifungu ambavyo vinakiuka uhuru wa vyombo vya habari na zimebinya uhuru wa kujieleza, sasa badala ya kwenda mbele tungerudi nyuma.

"Mfumo ulikuwa unataka kwenda ki-communist yaani tulitaka kwenda mfumo wa kijamaa na mfumo wa kijamaa ndani yake una utawala wa Kiimla, kwa maana ya dictatorship sasa element za dictatorship zinaleta chuki katika jamii.Mtu akiwa na jambo amekwazika na akakaa kimya maana yake anaumia na kiafya pamoja na kisaikolojia anapata madhara,"amefafanua Mwalimu Makuru.

Mwishoni mwa mwaka jana, Rais wa Mahakama ya Afrika, inayoshughulika na haki za binadamu, Jaji Imam Aboud, katika mafunzo ya wiki moja ya Majaji wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO) alisema,uhuru wa kujieleza, uhuru wa kutoa mawazo.

Sambamba na uhuru wa demokrasia na uhuru wa kutoa habari, vyote vinapaswa kutolewa katika misingi yenye kufuata sheria na haki ili kusiwepo na uvunjifu wa amani.

Jaji Aboud alisema vyote vikifuatwa haoni kama kutakuwepo na uvunjifu wa amani katika nchi za Afrika na kusisitiza kila mmoja kukumbuka wajibu wake wenye lengo la kulinda amani ya nchi husika.

Rais huyo alitoa wito wa kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu, akisema bado haki hizo zinavunjwa na kuuweka mashakani uhuru wa demokrasia katika nchi nyingi Afrika.

Alisema, uhuru wa vyombo vya habari na usalama wao ni jambo muhimu, linaloheshimu misingi ya utawala wa kisheria na demokrasia, hivyo majaji wana wajibu wa kuhakikisha wanahabari wanakuwa na uhuru wa kupewa habari na usalama wao katika nchi za Afrika.

Pia alisisitiza kwa wanahabari kuhakikisha wanafuata misingi ya uandishi wa habari zinazoeleza uhalisia na ukweli wa jambo, ili kuepuka kuleta mfarakano na machafuko ya ndani ama nchi kwa nchi.

“Mahakama za nchi katika Umoja wa Afrika, zinaweza kushirikiana na vyombo vya habari kutoa habari zinazohamasisha amani kuliko habari zenye kuleta mtafaruku,”alisema Rais Jaji Aboud.

Kwa sasa,Serikali inatarajiwa kuwasilisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016 katika vikao vya Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news