Wapitisha rasimu ya bajeti bilioni 30.6/- Njombe DC

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe limepitisha shilingi bilioni 30.6 kama rasimu ya bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Valentino Hongoli ameyabainisha hayo Januari 31, 2023 kwenye kikao cha bajeti cha halmashauri hiyo kilichofanyika wilayani Njombe.

Hongoli amesema, madiwani wanatakiwa kusimamia vizuri miradi inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo na kutenga fedha asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na asilimia 30 ya miradi ya maendeleo.

"Ili tuweze kutekeleza vizuri bajeti ijayo tunahitaji kukamilisha miradi yote ambayo tumeipanga hasa kupitia mapato ya ndani," amesema.

Pia amesema katika kutekeleza miradi ya kimkakati inatakiwa ushirikiano na usimamizi mkubwa wa makusanyo ya mapato na kupeleka fedha kwa wakati katika miradi.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo,Sharifa Nabalang'anya amesema kupitia bajeti hiyo wanatarajia kutekeleza na kubuni miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuongeza mapato ya halmashauri.

Amesema, kabla ya kupitishwa kwa bajeti hiyo asilimia 70 ya mapato ya ndani yalikuwa yanategemea eneo moja pekee la misitu, lakini sasa wanakwenda kuondokana na hali hiyo.

Amesema kutokana na mafunzo waliyoyapata baada ya kutembelea halmashauri za Chalinze na Dodoma yameleta matokeo makubwa na yameanza kuonekana kwa sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news