WAZIRI MAKAMBA AWATAKA WARATIBU WAPYA MIRADI YA UMEME VIJIJINI KUTOIANGUSHA SERIKALI

VERONICA SIMBA NA ISSA SABUNI-REA

WAZIRI wa Nishati, January Makamba amewaasa vijana walioajiriwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa nafasi ya Waratibu Miradi ya Umeme Vijijini kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi ili kulinda imani iliyooneshwa na Serikali kwao.
Baadhi ya Waratibu wapya wa Miradi ya Umeme Vijijini wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nishati, January Makamba (Meza Kuu-katikati) baada ya kuhitimisha mafunzo yao mafupi kuhusu namna bora ya kutekeleza kazi zao. Mafunzo hayo yamehitimishwa Februari 28, 2023 Dodoma yakihusisha vijana 136 waliofaulu usaili hivi karibuni.

Akizungumza leo Februari 28, 2023 jijini Dodoma, Makamba amewataka vijana hao 136 waliofaulu usaili wa nafasi husika, kwenda kuwatendea haki wananchi walengwa ambao ni wa maeneo ya vijijini nchi nzima, kwa kuhakikisha kiu yao ya kufikiwa na umeme inatimizwa na azma ya Serikali kufikisha nishati hiyo vijijini kwa wakati na ubora inatekelezwa kikamilifu.

Aidha, Waziri amewaasa waajiriwa hao wa Mkataba, kutojiona kuwa wao ni bora zaidi kwa vile tu wamepata nafasi hizo kati ya vijana takribani 3,000 waliotuma maombi bali waichukulie kama bahati ya kipekee na kuitumia fursa hiyo kudhihirisha kuwa kuchaguliwa kwao hakukufanyika kwa makosa.

“Wale wenzenu ambao hawakubahatika siyo kwamba hawakuwa na vigezo. Takribani wote waliotuma maombi walikuwa na vigezo lakini kutokana na nafasi zilizohitajika kuwa ni 136 tu, ndiyo maana wachache wenu kutoka kundi hilo mkabahatika. Ichukulieni fursa hii adhimu kuchapa kazi na kudhihirisha hatukufanya makosa kuwachagua,” amesisitiza.

Akizungumzia sababu za Serikali kuajiri vijana hao kwa wakati huu, Waziri amebainisha kuwa ni kwa ajili ya kuwezesha uharakishaji wa kutekeleza miradi ya umeme vijijini kwa uzuri, ubora na viwango vinavyotarajiwa, na kubainisha kuwa lengo ni kuhakikisha vijiji vyote Tanzania Bara viwe vimefikiwa na umeme ifikapo Desemba mwaka huu wa 2023.
Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na Waratibu wapya wa Miradi ya Umeme Vijijini wakati wa kuhitimisha mafunzo yao mafupi kuhusu namna bora ya kutekeleza kazi zao. Mafunzo hayo yamehitimishwa Februari 28, 2023 Dodoma yakihusisha vijana 136 waliofaulu usaili hivi karibuni.

Akifafanua, amesema kazi ya kupeleka umeme vijijini inaendelea vizuri ambapo hadi sasa takribani asilimia 80 ya vijiji vyote Tanzania Bara vimeshafikiwa na umeme lakini pamoja na takwimu hizo nzuri, kumekuwepo na uzorotaji na uchelewaji wa kupeleka nishati hiyo kwa baadhi ya vijiji kutokana na usimamizi hafifu.

Ameongeza kuwa, kwa kuwa Wakala wa Nishati Vijijini ni Mfuko, ambapo watendaji wake wanahusika zaidi na kutafuta Wakandarasi na kuwapa kazi ya kupeleka umeme huku usimamizi wa kazi hiyo ukifanywa na watu wengine, hilo limekuwa tatizo lililoibua malalamiko kutoka kwa wananchi wengi vijijini kuwa miradi inachelewa huku ikigubikwa na changamoto kadhaa.
“Kwa hiyo, ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hii kwa uzuri, ubora na viwango vinavyotarajiwa, Wizara kupitia REA tukaomba kibali maalumu serikalini, kuajiri Waratibu wa Miradi ya Umeme Vijijini katika kila Wilaya ili watusaidie na tunashukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ikaridhia.”

Akizungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi baadaye, Waziri Makamba amesema vijana hao watasaidia kuzunguka vijijini kuhakikisha kwamba umeme unafika kwa wakati mahali kote ambako Serikali imelenga kupeleka nishati hiyo. Aidha, watahakikisha wakandarasi wako eneo la kazi, vifaa vipo na kazi inafanyika.

Amesema kazi nyingine watakayoifanya vijana hao ni kusaidia kutoa taarifa za haraka zaidi kwa wananchi, inapotokea changamoto ya uchelewaji mradi pamoja na kufanya mawasiliano na viongozi mbalimbali wa maeneo husika kuanzia ngazi ya Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri ili wawe wanajua wakati wote nini kinaendelea katika maeneo hayo.

“Nia yetu sisi ni kwamba tuharakishe utekelezaji wa kupeleka umeme vijijini ili kufikia Desemba 2023, vijiji vyote viwe vimefikiwa na umeme, kwa sababu tayari kila kijiji kina Mradi, bajeti ipo na wakandarasi wako eneo la kazi. Shida yetu ilikuwa ni utekelezaji wa kasi ambapo vijana hawa watatusaidia kuhakikisha kasi inakuwepo.”
Katika hatua nyingine Waziri Makamba amewataka Waratibu Miradi hao kuhakikisha wanalinda taswira njema ya Serikali kwa kuwa na tabia njema pamoja na kujenga mahusiano mema na jamii iliyopo maeneo yao ya kazi wakiwemo viongozi mbalimbali na wananchi.

Amewapa hamasa kuwa uchapakazi, tabia njema na mahusiano mema na jamii vinaweza kuchangia Serikali kuridhia uhuishwaji wa mikataba yao ya kazi kwa kipindi kingine.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo mafupi kwa waratibu wapya wa Miradi ya Umeme Vijijini, Februari 28, 2023 jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nishati, January Makamba na kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka REA, Grace Sengula.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amemshukuru na kumpongeza Waziri Makamba kwa upatikanaji wa Waratibu hao wa Miradi akibainisha kuwa ndiye aliyetoa wazo husika na kulisimamia kuhakikisha linatekelezwa.

Amesema kupatikana kwa vijana hao kutawezesha Wakala kujiamini zaidi katika utendaji kazi wake kutokana na kuwa na uhakika kuwa miradi inayotekelezwa na Wakala inasimamiwa ipasavyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya wenzao, baadhi ya Waratibu Miradi wapya, Werema Mwita, Saada Ally na Saidi Mwijae wameishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa hiyo na kuahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii na weledi huku wakizingatia maelekezo yote waliyopewa na Waziri.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (mbele), wakimsikiliza Waziri wa Nishati, January Makamba (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na Waratibu wapya wa Miradi ya Umeme Vijijini wakati wa kuhitimisha mafunzo yao mafupi kuhusu namna bora ya kutekeleza kazi zao. Mafunzo hayo yamehitimishwa Februari 28, 2023 Dodoma yakihusisha vijana 136 waliofaulu usaili hivi karibuni.

Kwa muda wa siku mbili kuanzia jana, Februari 27, 2023, Waratibu Miradi hao 136 walikuwa wakipatiwa mafunzo mafupi na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo yalilenga kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Vijana hao wameajiriwa kwa Mkataba wa miezi mitatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news