BINTI:WEWE SI KAMA WENGINE-4

NA LWAGA MWAMBANDE

BINTI tambua kuwa,kujipenda wewe binafsi kutakusaidia namna sahihi ya kuwapenda wengine katika maisha ya kila siku.

Picha na lifestylebymo.

Ukizungumzia kuwapenda wengine tunajumuisha familia, ndugu, jamaa, marafiki, washirika, mumeo mtarajiwa na hata wale usiowajua kabisa.

Aidha, tambua kuwa, kujipenda kunahusisha kujithamini, kujijali, kujiheshimu na kujiamini pia, na tabia hizi zitaathiri pia namna unavyoishi na kuwachukulia wengine.

Pia utakapojipenda na kutambua maana halisi ya upendo na namna unavyoweza kumjenga mtu mwingine basi nawe utatamani na wengine wavune matunda ya upendo huo.

Na mara zote, hutatamani wadharauliwe wala washushwe thamani wasijaliwe au wakose ujasiri, ile hali ya kujipenda na furaha itokanayo na upendo huo itawaambukiza wote utakaokutana nao maana ndicho kilichoujaa moyo wako.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,wakati unaendelea kudumisha upendo kwa wengine yafaa kutambua kuwa, wewe si kama wengine bali una thamani kubwa,hivyo zidi kujiheshimu, kujithamini na kujinynyekeza mbele za Mungu. Endelea;


1. Kwa muonekano wako,
Hiyo ni turufu yako,
Ndiyo upekee wako,
Wewe si kama wengine.

2. Utunzavyo nywele zako,
Zilivyo kichwani kwako,
Hivyo ndivyo wewe uko,
Wewe si kama wengine.

3. Huo usukaji wako,
Huo ni mvuto wako,
Hakiki ni wa peke yako,
Wewe si kama wengine.

4. Kama uchanaji wako,
Nywele ni Afro yako,
Sifanye yenye vituko,
Wewe si kama wengine.

5. Ya kwako mabadiliko,
Kila mtindo ni wako,
Hushusha thamani yako,
Wewe si kama wengine.

6. Ijenge brandi yako,
Ya huko kichwani kwako,
Kuwe ni rejea yako,
Wewe si kama wengine.

7. Utunze ubora wako,
Usilete mcharuko,
Hiyo ni fedheha kwako,
Wewe si kama wengine.

8. Nywele zako sura yako,
Ni kuonekana kwako,
Tunza staili zako,
Wewe si kama wengine.

9. Na vipi mavazi yako,
Ni utambulisho wako?
Au waishi kivyako?
Wewe si kama wengine.

10. Vimini mapenzi yako,
Vyatawala mwili wako?
Ni muonekano wako?
Wewe si kama wengine.

11. Au matukio yako,
Na mabadiliko yako,
Kwamba viko na haviko?
Wewe si kama wengine.

12. Au ndefu nguo zako,
Hatuoni goti lako,
Ni kujisetiri kwako,
Wewe si kama wengine.

13. Nguo upekee wako,
Na hata heshima yako,
Pia ni kituko kwako,
Wewe si kama wengine.

14. Kutoeleweka kwako,
Pengine kaburi lako,
Na pia mkosi wako,
Wewe si kama wengine.

15. Tena na usingo wako,
Ni mawindo na msako,
Macho yaangaza kwako,
Wewe si kama wengine.

16. Kwa kueleweka kwako,
Hata hizo nguo zako,
Pengine upenyo wako,
Wewe si kama wengine.

17. Wengine waache huko,
Wafanyayo siyo yako,
Tafuta upeke wako,
Wewe si kama wengine.

18. Kifwata wengine huko,
Wala hunacho cha kwako,
Tofauti na wenzako,
Wafanana na wengine.

19. Wabana nafasi yako,
Na hata mpenyo wako,
Kutoka kwa Mungu wako,
Wafanana na wengine.

20. Umeumbwa peke yako,
Wavamia ya wenzako,
Kwani usiwe na yako?
Wewe si kama wengine.

21. Yajali maisha yako,
Hata mwelekeo wako,
Lizaliwa peke yako,
Wewe si kama wengine.

22. Unayo maisha yako,
Ukifwata njia yako,
Bila kuiga wenzako,
Wewe si kama wengine.

23. Tuone ubora wako,
Tuhisi uwepo wako,
Tupende uwepo wako,
Wewe si kama wengine.

24. Mapenzi ya Mungu wako,
Katika maisha yako,
Yawe ndiyo mwanga wako,
Wewe si kama wengine.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Utenzi huu ni sehemu ya Mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana (0752 352 116) wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo ameyatoa katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya Mabinti. Mashairi yatakujia katika sehemu saba.

Post a Comment

0 Comments