JWTZ latangaza nafasi za kujiunga na jeshi, tazama vigezo hapa

NA DIRAMAKINI

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kujiunga na jeshi hilo kwa vijana ambao wametumikia au wamefanya mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa miaka miwili kisha wakarejeshwa majumbani.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda akiwa Dodoma leo amesema, “Vijana hawa walifanya mafunzo JKT na walipotimiza miaka miwili wakapewa vyeti baada ya kukosa fursa aidha kuandikishwa JWTZ au katika Taasisi/Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, walirejeshwa majumbani, lakini sasa fursa imepatikana, naishukuru Serikali tumepata nafasi kuandikisha Vijana hawa”

“Kijana anatakiwa awe Raia wa Tanzania wa kuzaliwa umri wa miaka 18-26 kwa Form IV hadi Form VI, kwa wenye elimu ya juu kufikia shahada ya uzamili umri usizidi miaka 27, awe na afya nzuri ya mwili na akili, tabia njema, nidhamu nzuri na awe hajawahi kupatikana na kosa la kijinai au kushtakiwa Mahakamani na kufungwa, vilevile awe na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya Shule na taaluma na pia awe hajawahi kutumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo na awe na cheti cha kuhudumia JKT kwa miaka miwili," amefafanua, fuatilia muongozo hapa
chini;

 

JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA

NAFASI ZA KUJIUNGA NA JESHI

1.Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linatangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa Vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kuanzia Kidato cha Nne hadi Shahada ya Uzamili ambao wamemaliza Mkataba wa Mafunzo ya Kujitolea JKT na kurudishwa majumbani.

SIFA ZA MWOMBAJI

2.Vijana wa Kitanzania wenye nia ya kuandikishwa Jeshi wanatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-

a.Awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa mwenye Kitambulisho cha Taifa.

b.Awe na umri wa miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya Kidato cha Nne hadi Kidato cha Sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya Juu.

c.Awe na afya nzuri na akili timamu.

d.Awe Mtanzania mwenye tabia na nidhamu nzuri, hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai Mahakamani na kufungwa.

e.Awe na cheti halisi cha kuzaliwa (Original Birth Certificate), vyeti vya Shule na vyeti vya Taaluma.

f.Awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM).

g.Asiwe ameoa au kuolewa.

h.Awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mkataba wa kujitolea miaka miwili (2) na kutunukiwa cheti. Wale vijana wa JKT waliopo Makambini ambao wana sifa tayari, utaratibu wao wa kuwaandikisha unafanyika tofauti na vijana waliopo majumbani ambao tangazo hili linawahusu.

UTARATIBU WA KUTUMA MAOMBI

3.Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi Dodoma kuanzia tarehe ya tangazo hili hadi tarehe 20 Machi, 2023 yakiwa na viambatisho vifuatavyo:-

a.Nakala ya Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA.

b.Nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya Shule na Chuo.

c.Nakala ya cheti cha JKT.

d.Namba ya simu ya mkononi ya mwombaji.

MAOMBI YATUMWE KWA ANUANI IFUATAVYO

4.a.Mkuu wa Utumishi,

Makao Makuu ya Jeshi,

Sanduku la Posta 194,

DODOMA, Tanzania.

b.Email: ulinzimagazine@tpdf.mil.tz

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news