Kamati ya Bunge yatoa maagizo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL)

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha kitengo cha masoko kinaanza kutafuta kampuni za kusafirisha mzigo kwenye meli zinazojengwa na kufanyiwa ukarabati ili kuziwezesha meli hizo kuanza kazi mara moja baada ya ujenzi na ukarabati kukamilika.
Akizungumza mkoani Kigoma mara baada ya kukagua mradi wa ukarabati wa meli ya MT. Sangar na eneo ambalo litajengwa chelezo kipya, Mhe. Jerry Silaa amesema, uwekezaji wa fedha uliowekwa hususani kwenye miradi ya ujenzi na ukarabati wa meli unawapa jukumu kampuni hiyo kuhakikisha wanapata mzigo wa uhakika utakaowawezesha kupata fedha na hatimaye kuanza kujilipa mishahara na kuendesha kampuni bila kutegemea fedha kutoka Serikalini.

“Serikali imeshaweka fedha nyingi kwenye kampuni hii, na kamati yetu ina jukumu la kuhakikisha mnapata fedha za kuweza kujiendesha wenyewe pasipo kutegemea ruzuku kutoka Serikalini, mtafanikiwa kupata fedha mtaanza huduma za kusafirisha mizigo kupitia meli hizi,’ amesema Mhe. Silaa.

Mhe. Silaa ameitaka bodi hiyo kumlipa Mkandarasi Kampuni ya KTMI ambayo ndio yenye kandarasi ya kujenga meli hiyo ili kuepuka madeni ambayo yanaweza kuzalishwa kutokana na kucheleweshwa kwa malipo.

Aidha, Mwenyekiti Mhe. Silaa ameipongeza Bodi, Menejimenti na Watumishi wa Kampuni hiyo kwa kusimamia vyema miradi inayotekelezwa na kuhakikisha wahandisi wake wanapata ujuzi ili kuweza kusimamia vyema meli hizo mara baada ya ujenzi na ukarabati kukamilika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya MSCL, Meja Jenerali mstaafu John Mbungo amemuhakikishia Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Mhe. Silaa kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na tayari Kampuni imeshaweka mpango wa muda mfupi na mrefu kwa wa namna fedha iliyowekezwa inaweza kurudi kwa kuhakikisha mzigo wa uhakika unapatikana.

Naye Mtendaji Mkuu wa MSCL, Eric Hamis amesema mradi wa ukarabati wa MT. Sangara unatekelezwa na Kampuni ya KTMI kutoka nchini Korea Kusini kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 8 na kwa sasa umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mapema mwezi April mwaka huu.

Eric ameongeza kuwa miongoni mwa matokeo ya ukarabati huo mkubwa ni pamoja kupungua kwa masaa ya safari ambapo utaiwezesha meli hiyo kusafirisha mzigo kwa saa 6 tu ukilinganisha na hapo kabla ambapo ilikuwa inatumia saa zaidi ya 15 kwa safari moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news