KAZI MKONO KINYWANI:Zile zilizo halali,Hata zisizo na kozi, huleta ndizi na wali mezani

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa Isaack Zake ambaye ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, kupitia moja ya makala zake za hivi karibuni alieleza kuwa, kwa tafsiri isiyo rasmi tunaweza kusema kazi ni shughuli inayohusisha akili au nguvu za mwili kwa lengo la kufikia kusudi au kupata matokeo yaliyokusudiwa.
Aidha, kwa kuitazama tafsiri hiyo ya kazi tunaweza kupata mambo kadhaa ikiwemo kusudi au lengo, kwani ili kazi iwepo ni lazima kuwe na kusudi au sababu ya mtu kufanya au kutaka kufanya kile anachofanya. 

Pia, ili kazi iwepo ni lazima mtu awe na sababu kwa nini anatumia akili yake au nguvu zake kufanya anachofanya popote pale alipo.

Vile vile kuna matumizi ya akili au nguvu, kwani kazi inahusisha matumizi ya akili au nguvu au vyote kwa pamoja yaani akili na nguvu. 

Haitoshi tu kuweka lengo au kuwa na kusudi lazima hatua zichukuliwe kufanya kitu kwa kutumia akili na nguvu ili kupata matokeo yanayotarajiwa.

Jambo lingine ni matokeo ambayo ni zao la kazi. Yapo matokeo ya aina nyingi inategemea kusudi la mtenda kazi alilokuwa nalo kabla hajawekeza akili na nguvu zake katika kazi husika. 

Mtu anaweza kupata matokeo ya furaha kama lengo ilikuwa kufurahi au kuona wengine wakisaidika kama lengo ilikuwa kutoa msaada kwa kazi yake au kupata fedha kama lengo la kazi ilikuwa fedha.

Aidha,mtu akisema anafanya kazi maana yake ana kusudi ndani yake ambalo analifikia kwa kuweka akili yake na nguvu zake kwenye matendo ili hatimaye apate matokeo aliyokusudia. 

Hivyo mtu yeyote mwenye lengo au kusudi na kuwekeza muda wake akili yake na nguvu zake kuhakikisha anafikia lengo lake basi huyo ni mfanyakazi au mtenda kazi. Mshairi wa kisasa Lwaga Mambande anasititiza kuwa, penye bidii, ubunifu na kufanya kazi halali, lazima ufurahie matokeo bora. Endelea;

1. Kazi jamani ni kazi, bora tu iwe ni halali, 
Hili tuliweke wazi, na tena ndio ukweli, 
Acha kudharau kazi, kwa kuangalia hali, 
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha. 

2. Zamani tunakumbuka, tulikuwa na methali, 
Sasa hizo tumechoka, haziendani na hali, 
Mambo zilizoyacheka, sasa ni kazi halali, 
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha. 

3. Kwa kuokota makopo, zamani hatari kweli, 
Mtu alikuwa popo, ya kwamba hana akili, 
Leo ni ajira ipo, yaleta pesa halali, 
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha. 

4. Chupa tupu kuokota, watu wanapata mali,
Kama wanapitapita, juu jua liko kali,
Ndiyo hivyo watafuta, waweze kufika mbali,
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha.

5. Kuendesha bodaboda, hiyo ni kazi halali, 
Watu wapoteza muda, huo mtaji kamili, 
Wajiondolea shida, maisha yawa ya ghali, 
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha. 

6. Hao wenye bodaboda, hizo pikipiki mali, 
Hapo wanapata ada, na nyumba zenye kivuli, 
Maisha si kawaida, wanazidi kuwa ghali, 
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha. 

7. Anayedharau kazi, za bodaboda halali, 
Apuuzwe mpuuzi, aonekana katili, 
Yake eti ndiyo kazi, za wengine ni batili, 
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha. 

8. Enyi wenye bodaboda, hata guta ni halali, 
Wala msione shida, kuendeleza shughuli, 
Utaosema ni muda, mnaweza fika mbali, 
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha.

9. Hebu tuheshimu kazi, zile zilizo halali,
Ambazo watenda kazi, wajipatia ugali,
Hata zisizo na kozi, huleta ndizi na wali,
Kazi mkono kinywani, ni halali kwa maisha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news