Maagizo ya Rais Dkt.Mwinyi yagusa kila mmoja Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuendelea kufanyiana wema, hisani, kuishi kwa kupendana na kusaidiana kama Mwenyenzi Mungu alivyoamrisha katika Quran Tukufu.

"Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tumehimizwa tuongeze bidii katika kufanyiana wema, hisani, kuishi kwa kupendana na kusaidiana kama Mwenyenzi Mungu alivyotuamrisha katika haya mbalimbali za Quran Tukufu na kusisitizwa katika hadithi za Mtume Muhammad S.A.W, bila shaka kwa kufanya hivyo, Mwenyezi Mungu atatulipa malipo mema na kutuongezea baraka katika nchi yetu;

Ameyasema hayo usiku wa Machi 22, 2023 kupitia salamu zake kwa wananchi za kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Mwaka 1444Hijriya,sawa na Mwaka 2023 Miladia.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amefafanua kuwa,kufanya hayo ni misingi muhimu ya kuondoa chuki,husda, dhuluma na kuleta furaha na ustawi katika jamii.

"Ndugu wananchi katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tunapaswa kuzingatia pia umuhimu wa kudumisha amani, na utulivu tulionao, kwa hakika ibada ya swaumu pamoja ibada nyingine tunazozifanya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zinahitaji sana kuwepo kwa amani na utulivu.

"Kwa hivyo, sote kwa pamoja tuna wajibu wa kusimamia amani na utulivu ili tupate wasaa mzuri wa kutekeleza ibada zetu, tujiepushe na mambo yote ambayo yanaweza kupelekea uvunjivu wa amani na kusababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaoitembelea nchi yetu.

"Tudumishe utamaduni wetu wa kuheshimu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuacha kufanya mambo ambayo yanaweza kusababisha maudhi au kuleta karaha kwa waliofunga,tuendelee kuishi kwa kuvumiliana na kuheshimu dini, jambo ambalo limechangia kudumu kwa amani ya nchi yetu,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa, "Kama sote tunavyofahamu katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mahitaji katika familia zetu yakiwemo ya bidhaa za chakula na vitu vingine, huongezeka.

"Tunamshukuru Mwenyenzi Mungu kwamba licha ya kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa za chakula duniani. kulikosababishwa na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wetu, Serikali imejiridhisha kuwepo kwa bidhaa za kutosha za chakula hapa nchini, katika maghala mbalimbali ya wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza bidhaa hizo, kwa mnasaba huo hakuna haja ya wananchi kuwa na hofu ya upatikanaji wa chakula katika kipindi chote cha Mwenzi Mtukufu wa Ramadhani,"amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara na kuwataka kuuza bidhaa kulingana na bei elekezi ya Serikali, kwa yule ambaye atakaidi kufanya hivyo, atachukuliwa hatua za kisheria.

"Wito wangu kwa wafanyabiashara wauze bidhaa hizo kwa bei elekezi ya Serikali na kuacha kuficha bidhaa hizo ili kusababisha upungufu na kupandisha bei. Kama nilivyosema wakati nikizungumza na waandishi wa habari Februari 28, mwaka huu kitendo hicho hakitavumiliwa.

"Na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria, naomba wananchi mtoe ushirikiano kwa vyombo vinavyohusika katika kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anakwenda kinyume na maagizo haya,"amesisitiza Rais Dkt.Mwinyi na kuagiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news