NA MWANDISHI WETU
MKUTANO wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umefunguliwa Machi 13, 2023 jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika mkutano huo, ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi.Amina Shaaban.
Wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda wa DRC,Balozi Songhu Kayumba alisisitiza umuhimu wa wajumbe kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yatakayolenga kufanikisha utekelezaji wa ajenda zitakazojadiliwa.
Makatibu wakuu wanajadili ajenda mbalimbali ambazo ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Maamuzi ya Wakuu wa Nchi na Serikali waliyotoa katika mikutano iliyopita.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki kikamilifu kwenye mkutano huo na imejipanga kusukuma utekelezaji wa ajenda ilizoziibua au kuziunga mkono katika mikutano iliyopita.
Ajenda hizo ni pamoja na ujenzi wa sanamu ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo itasimikwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU).
Sambamba na mpango wa Kanda wa Ununuzi wa Pamoja wa Bidhaa za Afya unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na mkakati wa pamoja wa Kanda wa Kusimamia Sekta ya Mbolea.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt.Stergomena L.Tax (Mb) anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika kuanzia Machi 18 hadi 20, mwaka huu baada ya Mkutano wa Makatibu Wakuu kukamilika.