Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete aielekeza Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) kujenga nyumba za watumishi kwenye maeneo yenye fursa

NA MARY MWAKAPENDA

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameielekeza Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) kujenga nyumba za watumishi kwenye maeneo yenye fursa na mazingira mazuri ya kuishi ili kuwawezesha watumishi wote hata walio kwenye maeneo ya pembezoni kupata makazi bora ya kuishi yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa WHI Dar es Salaam.

Mhe. Kikwete ametoa maelekezo hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Watumishi Housing Investments jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kikwete amesema pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Watumishi Housing Investments, ni vizuri zaidi wakafikiria kujenga nyumba nyingi zaidi maeneo yenye uhitaji mkubwa wa nyumba hizo, akitolea mfano wa maeneo ya pembezoni mwa nchi ambayo ndio yenye uhitaji mkubwa wa nyumba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

“Mnafanya kazi nzuri sana ya ujenzi wa nyumba hizi, lakini mnatakiwa kuangalia fursa, maeneo gani yana uhitaji mkubwa wa nyumba, hasa maeneo ya pembezoni ili hata wanaohamishiwa huko wafurahie maisha na kutekeleza kikamilifu jukumu la kutoa huduma bora kwa wananchi,” Mhe. Kikwete amesisitiza.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, pamoja na haki na stahiki nyingine wanazopata watumishi, mazingira mazuri ya kuishi ni jambo lingine la msingi ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na WHI wakati wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wa umma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa WHI jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kikwete amesema ni matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona watumishi wa umma wanafanya kazi kwa bidii na maarifa, hivyo katika kufikia malengo ya Mhe. Rais, Watumishi Housing Investments wana nafasi kubwa ya kuunga mkono lengo hilo la Mheshimiwa Rais kwa kujenga nyumba bora kwa ajili ya kuziuza na kuwapangisha watumishi wa umma nchini.
Sehemu ya Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa WHI jijini Dar es Salaam.

“Taasisi zinazojenga nyumba ziko nyingi, wengine wanajikita kwenye ujenzi wa nyumba kwa ajili ya mwananchi yeyote lakini sisi Watumishi Housing Investments tuna malengo yetu ambayo yamejikita kwa watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, hivyo tunapaswa kuhakikisha malengo ya taasisi yanatimia.

Mhe. Kikwete ameisisitiza Menejimenti ya taasisi hiyo kutosita kuwashirikisha Viongozi na Menejimenti ya Ofisi ya Rais, menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pale wanapokutana na changamoto au kama kuna mwongozo wowote wanaouhitaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akifurahia jambo wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) akiwa kwenye ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Kikwete ameitaka taasisi hiyo kutangaza utekelezaji wa majukumu ya taasisi yao ili yafahamike kwa wahusika.

“Watumishi wanahitaji kuyajua majukumu yenu, mjitahidi kujitangaza ili kuwafikia kiurahisi tunaowalenga na kuifanya taasisi yetu kuwa kimbilio la watumishi pale wanapohitaji kuwa na nyumba iwe ya kununua au kupangisha,” Mhe. Kikwete amefafanua.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimizia uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi za umma zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news