Mradi wa Shule Bora wakoleza kasi ya mageuzi ya elimu nchini, wizara yanena

NA GODFREY NNKO

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Dkt.Franklin Jasson Rwezimula amesema, Serikali kupitia wizara hiyo itaendelea kutenga fedha nyingi na kuweka mazingira bora kwa wahisani wakiwemo wadau wa elimu ili waweze kushiriki katika jitihada za kuboresha elimu nchini.
Dkt.Rwezimula ameyasema hayo leo Machi 24, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa wahariri wa vyombo vya habari na mameneja nchini kuhusu Mradi wa Shule Bora ambao umelenga kuweka mazingira salama shuleni katika ngazi ya awali na msingi.

Mradi wa Shule Bora unalenga katika mambo manne ikiwemo watoto wote kujifunza shuleni, kufundisha, watoto wote wa Kitanzania shuleni kuwa katika mazingira salama na rafiki ili kuwawezesha kumaliza elimu ya msingi na kuendelea na elimu ya sekondari (jumuishi) na kuimarisha mfumo wa elimu.
Amesema, Mradi wa Shule Bora unatekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara ukiwemo Dodoma, Katavi, Rukwa,Singida, Mara, Simiyu, Pwani,Singida, Tanga na Kigoma. 

Naibu Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa, kupitia mradi huo, jumla ya halmashauri 67, shule za msingi 5757, wanafunzi milioni 3.8 na walimu 54,000 watanufaika na utekelezaji wake. 
Dhamira ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo wahariri wa habari nchini ili waweze kuufahamu kwa kina Mradi wa Shule Bora nchini ambao unatekelezwa katika mikoa hiyo.

"Lengo letu ni kuhakikisha mnaifahamu programu hii, ili waandishi wanapoleta taarifa, muweze nanyi kwanza kuelewa. Huu ni mwendelezo wa utoaji wa elimu hii, kwani ulianza na waandishi waliopo katika mikoa ambayo mradi unatekelezwa hapa nchini,"amefafanua Naibu Katibu Mkuu huyo.

Amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kikubwa katika Sekta ya Elimu katika kuhakikisha dhima ya Serikali ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu ili kuongeza ufanisi na kuongeza uzalishaji wa viwanda kwa maendeleo ya watu. 
"Mtaji mkubwa wa kuendeleza kasima hiyo umewekwa katika kuendeleza rasilimali watu, kuanzia elimu ya awali na msingi. 

"Wizara yetu inaanzia kutoa elimu kuanzia elimu ya awali mpaka wale watu ambao wameshastaafu, kuna programu za aina mbalimbali. Wizara yetu ina taasisi zaidi ya 30 ambazo zinatoa elimu mbalimbali, zinazotoa hadi elimu ya watu wazima.Kwa hiyo, wizara yetu ina umuhimu mkubwa. 

"Uandaaji wa rasilimali watu pamoja na mambo mengine unajumuisha uandaaji na uendelezaji wa programu na michakato mbalimbali inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimali watu nchini. 
"Kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuwawezesha vijana kushiriki katika kujenga uchumi mara tu baada ya masomo. Hii ni pamoja na kuboresha viwango vya utoaji wa elimu msingi, ufundi na mafunzo ya ufundi 

"Ili kutekeleza hayo Serikali imeendelea kutenga fedha na kuweka mazingira vutivu kwa wahisani na wadau mbalimbali wa elimu kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali.
"Kutokana na jitihada hizo,sekta ya elimu imeweza kupokea programu mbalimbali katika ngazi ya elimu ya msingi, sekondari,vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu. Programu ya Shule Bora ni miongoni mwa programu hizo. Programu ya Shule Bora ni programu ya Serikali inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza la UK Aid,"amesisitiza. 

Aidha, Dkt.Rwezimula amewataka waratibu wa mradi huo kushirikisha vyombo vya habari katika kila hatua ili waweze kuwaeleza wananchi kinachojiri.
"Kwa sasa kama mnavyojua Serikali ipo kwenye kufanya mageuzi makubwa ya elimu nchini katika ngazi mbalimbali,huu mradi wa shule bora nao ni muendelezo wa mikakati wa kuboresha elimu,"amesema Dkt.Rwezemula.

Pia amewashukuru wadau mbalimbali wa elimu kutoka ndani na nje ya nchi katika jitihada zao za kuhakikisha wanaunga mkono maboresho mbalimbali ya sekta ya elimu ambayo yanaendelea kufanyika hapa nchini ikiwemo Serikali ya Uingereza. 
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka UK Aid, Bi. Lorah amefafanua kuwa, Mradi wa Shule Bora umelenga kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kuinua kiwango cha elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote wa kike na wa kiume katika shule za Serikali.

Amefafanua kuwa, mradi huo pia unawezesha watoto ambao wanatoka katika mazingira magumu kupata elimu sawa kupitia mazingira yaliyoboreshwa shuleni.
Pia amesema,kwa ushirikiano na Serikali mradi huo unafanya maboresho yatakayowezesha kila mtoto kupata msingi mzuri katika elimu yake ya awali, ili kuitumia fursa kwa kutoa mchango wake katika ukuaji wa nchi na maendeleo yake.

"Tunaamini mpango huo utaboresha matokeo ya masomo kwa watoto wote, kuboresha viwango vya mpito kwenda shule ya sekondari kwa wasichana, kupunguza ukatili wa kijinsia ndani na nje ya shule, na kuwasaidia watoto wenye ulemavu kupata elimu bora,"amebainisha. 
Aidha, amefafanua kuwa, mradi huo unatoa moja kwa moja mbinu bunifu za kuboresha ubora wa elimu katika mikoa tisa ya Tanzania kupitia wasimamizi,na itafanyika tathmini ya ujifunzaji.
Hata hivyo, Mradi wa Shule Bora chini ya ufadhili wa UK Aid unalenga kuunga mkono miradi ya elimu nchini huku ukipokea utaalamu wa kiufundi kutoka Cambridge Education.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news