Mwinjilisti Temba: Ndani ya miaka miwili, Rais Dkt.Samia ametuheshimisha kila sekta

NA DIRAMAKINI

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio Penuel ya Marangu mkoani Kilimanjaro, Alphonce Temba amesema, miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Taifa limeshuhudia mafanikio makubwa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kudumisha amani, umoja na mshikamano.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametimiza miaka miwili ya uongozi wake Machi 19, 2023 tangu aapishwe Machi 19, 2021 kuiongoza Serikali ya Awamu ya Sita kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ambacho kilitokea Machi 17, 2021 wakati akiendelea na matibabu jijini Dar es Salaam.

Ndani ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanikiwa kuiongoza nchi kwa umahiri mkubwa na kudumisha amani, upendo, utulivu na mshikamano kwa Watanzania.

Aidha, imekuwa ni miaka miwili ya mafanikio, matumaini, faraja na matarajio makubwa kwa Watanzania kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Serikali na ushirikiano mkubwa ambao Serikali imeupata kutoka kwa wananchi.

Watanzania wameshuhudia utekelezaji wa kasi wa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya kimkakati kwa Taifa letu inayojumuisha ujenzi reli ya kisasa, miradi ya umeme,usafirishaji wa majini, nchi kavu na angani,ujenzi wa ofisi za Serikali makao makuu Dodoma na uwekezaji katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Pia Watanzania wameshuhudia kuimarishwa kwa huduma za afya kutokana na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, ujenzi wa miundombinu ya elimu ukiwemo ujenzi wa madarasa, maabara na nyumba za walimu, ujenzi wa miradi ya maji, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme na kuimarisha kwa maeneo ya kutolea huduma.

Mbali na hayo Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amefanya kazi kubwa ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na mataifa mengine duniani kote, hali ambayo imeiwezesha nchi kunufaika na fursa mbalimbali za uhusiano huo ikiwemo kukuwa kwa biashara, kupata misaada katika maeneo mbalimbali,kupata mikopo yenye masharti nafuu na kukuza teknolojia na ujuzi.

Temba ambaye pia Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa ameyabainisha hayo wakati akielezea namna ambavyo, miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia ulivyotekeleza mambo mengi huku matarajio ya siku za mbeleni yakiwa makubwa zaidi kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ndani ya miaka miwili ametekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati na hakuna mradi uliosimama.

"Kila mmoja wetu ameshuhudia, lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuboresha viwango vya maisha ya kila Mtanzania na nchi hii imefanikiwa sana kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi wake.

"Miradi mbalimbali ya maji kwa wananchi imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa mijini na vijijini. hii ni hatua na ishara kuu ya kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inamtua Mama ndoo kichwani.

"Vivyo hivyo, juhudi kubwa sana zimefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kama kuimarisha ukusanyaji mapato ya Serikali na kuminya mianya ya upotevu wa fedha na kufanya ongezeko kubwa la fedha za umma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, kwa hiyo hii miaka miwili ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ni shangwe kila kona nchini,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Pia, Mwinjilisti Temba amefafanua kuwa, Rais Dkt.Samia ameonesha dhamira yake njema ya kulifanya Taifa kuwa na amani na mshikamano ikiwa ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote lile duniani.

Wakati huo huo, Mwinjilisti Temba amewashauri viongozi na watendaji mbalimbali wanaomsaidia Rais Dkt.Samia kuanzia ngazi za chini hadi juu kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo kwa weledi, bidii na kuzingatia ubora ili iweze kudumu.

"Mheshimiwa Rais Dkt.Samia, ni mama mwenye upendo,kwa Taifa na wananchi wake, ndiyo maana unaona miradi mikubwa mikubwa ikienda kwa kasi nchini. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia hivi karibuni amepelea zaidi ya shilingi bilioni 70 kutekeleza Mradi Mkubwa wa Maji wa Butimba.

"Huu ni mradi ambao utakapokamilika unatarajia kuzalisha zaidi ya lita milioni 48 kwa siku na unatarajiwa utasaidia kuondoa adha ya maji hasa kwa wananchi wanaoishi kwenye miinuko mkoani humo.

"Vile vile, Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), lililopo wilayani Rufiji mkoani Pwani, kila mmoja wetu anatambua kwa sasa kinachoendelea ni ujazazi wa maji, vyivyo hivyo ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea unakwenda kuiunganisha Tanzania kibiashara na nchi jirani zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

"Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Uganda, kwa hiyo Serikali ya Awamu ya Sita inafanya mambo makubwa kwa ustawi bora wa Taifa letu, ni faraja kubwa sana kuona Tanzania inakwenda kuwa kinara katika usafirishaji mizigo na kuokoa muda kupitia reli ya kisasa ambayo ni nyenzo muhimu ya kuhifadhi na kutunza barabara zetu,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Ametaja miradi mingine kuwa ni Ujenzi wa Meli ya kisasa ya MV Mwanza na Daraja la Kigongo- Busisi, kukamilisha Daraja la Tanzanite.

Sambamba na ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Uvuvi-Kilwa ambayo itatumia zaidi ya shilingi bilioni 266.7 kwa jili ya kupaisha shughuli za uvuvi, kufungua fursa za ajira kupitia Bahari ya Hindi.

Miradi mingine ni Bandari kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani ambapo kwa sasa kuna ujenzi mkubwa wa karakana kuu ya matengenezo ya treni na ujenzi mkubwa wa viwanda zaidi ya mia mbili unaendelea maeneo hayo ya Kwala.

"Tunaomba mipango miji ifanye haraka maana wananchi wanauziama maeneo kwa kasi kubwa na kuanza ujenzi bila kufuata taratibu za mipango mji, hivyo ni hatari sana kwa makazi holela wakati itakuwa ni kituo cha uwekezaji Afrika Mashariki na Kati."Mheshimiwa Rais Dkt.Samia anategemewa kufungua shughuli hizo za bandari kavu wakati wowote àu kumtumia mwakilishi, hongera sana mama kwa kuupiga mwingi na Tanzania kupaa kiviwanda na kiuchimi Afrika,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news