Kamati ya Bunge yatoa maelekezo kwa Mkandarasi wa reli ya kisasa

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe, Seleman Kakoso amemtaka Mkandarasi wa reli ya kisasa kwa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro na Makutopora kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ili aweze
kukamilisha mradi kwa wakati na muda uliopangwa.
Mhe.kakoso ameyasema hayo wakati kamati ya kudumu ya bunge ya miundombinu ilipokagua reli ya kisasa ya mwendokasi, kipande cha Dodoma-Makutupora na baadae Makutopora-Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

“Tunajua wakati mradi huu wa reli ya kisasa unaanza kulikuwa na changamoto nyingi na ndiyo kwanza miradi ya namna hii ilikuwa inaanza kutekelezwa nchini, lakini sasa Mkandarasi Yapi Merkezi ameshapata uzoefu wa kutosha na Serikali imemuongezea vipande vingine sasa ni jukumu lake kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ili huu mradi ukamilike haraka kwa mustakabali wa maendeleo ya sekta zingine na Taifa kwa ujumla kwani huu ni mradi wetu wa kimkakati kama Nchi,”amesisitiza Mhe.Kakoso

Akijibu maswali ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mhe. Atupele Mwakibete amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaeendelea kuwekeza kwenye ujenzi na maboresho mbalimbali ya miundombinu ya reli ya kisasa SGR na ile ya kawaida-MGR nchini ili kuboresha Sekta ya Usafiri na Usafirishaji kwa njia ya reli katika kukuza uchumi.

“Serikali inafanya jitihada za kujenga na kuboresha sekta ya reli nchini na hata kujenga reli mpya za kisasa na kawaida kwa mikoa ambayo hapo awali haikuwa na reli kwa mfumo wa Public-Private partnership, ambapo mpaka sasa mazungumzo na wakandarasi yanaendelea ya ujenzi huo kwa maeneo ya Mtwara-Mbambabay itakayokuwa na urefu wa kilometa 1,000, Tanga –Arusha kilometer 1,028, na Dar es salaam commuter network itakayokuwa na kilometa 1,600,” amesisitiza Mhe.Mwakibete.

Awali akitoa salamu za ukaribisho Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Bi. Amina Lumuli ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa utekelezaji wa majukumu yake kwa shirika kwani imekuwa chachu kwa shirika kufanya vizuri na kuendelea kuimarika kiutendaji

B.Amina amesema utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa awamu mbalimbali umekumbwa na changamoto mbalimbali kama vile mlipuko wa uviko-19 ambapo baadhi ya wafanyakazi waliondoka eneo la mradi ili kujiuguza na sasa vita vya Ukraine ambayo imeendelea kudhoofisha maendeleo ya mradi kwani mkandarasi vifaa vyake vingi anategemea kuagiza nje ya nchi, hivyo Kuchangia kupunguza ufanisi wa utekelezaji wa mradi.

Huu ni muendelezo wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikiwa ni maandalizi ya kikao cha 11 cha Bunge kinachotarajiwa kuanza Aprili 4, 2023 jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news