NCHI ZA SADC ZAWEKA MIKAKATI YA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

NA MWANDISHI WETU

MKUTANO wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimidhwa jijini Kinshasa tarehe 19 Machi 2023, huku agenda za kujikwamua kiuchumi katika kanda hiyo ya Kusini mwa Afrika zikipewa kipaumbele
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kushoto) pamoja na Mawaziri wenzake wakiwa wamesimama kwa ajili ya kuimba nyimbo za Taifa wakati wa hafla ya ufunguzi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaotathmini utekelezaji wa mipango ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mipango ya Mwaka wa Fedha 2023/2024, umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akisaidiana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde (Mb).

Maeneo ambayo Mhe. Waziri Tax alichangia wakati taarifa za utekeleaji zilipokuwa zinawasilishwa ni pamoja na hatua iliyofikiwa kuhusu tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili, ujenzi wa Sanamu la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mpango wa Kanda wa ununuzi wa pamoja wa vifaa vya afya unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Mhe. Waziri Tax alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utekelezaji wa maeneo hayo, kufuatia maelezo kuwa utekelezaji wa tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili upo katika hatua za kumpata mzabuni wa kufanya kazi hiyo na ujenzi wa Sanamu la Baba wa Taifa unaendelea, na kazi hiyo inatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2023. Kuhusu Mpango wa Kanda wa ununuzi wa pamoja wa vifaa vya afya, Dkt. Tax alisema MSD inaendelea na jukumu hilo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuongeza kasi ya kuitumia bohari hiyo ya dawa kwa kuwa manufaa yake ni makubwa hususan katika kupunguza gharama za ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Waheshimiwa Mawaziri na wajumbe wengine wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakifuatilia hotuba wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

Awali, wakati wa hafla ya ufunguzi, hotuba za viongozi ikiwa ni pamoja na; Waziri Mkuu wa DRC, Mhe. Jean-Michel Nyenge; Waziri wa Mtangamano wa Kikanda wa DRC na Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mhe. Didier Mazenga Mukanzu na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi ziliainisha maeneo muhimu ya kuwekewa mkazo ili kupanua wigo wa mtangamano na kuongeza kasi ya maendeleo baina ya nchi wanachama. 

Maeneo hayo ni pamoja ujenzi wa miundombinu, ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa za madini, ngozi na kilimo, kuwa na nishati ya umeme ya uhakika, usawa wa kijinsia katika siasa na zaidi ya yote ni umuhimu wa kuimarisha amani na usalama katika kanda.

Ilielezwa kuwa maeneo hayo yameainishwa vyema katika Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (2020-2030) ambapo Sekretarieti ya SADC imeahidi kuendelea kuratibu na kuhamasisha utekelezaji wake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Waziri wa Zambia wakati waliposhiriki hafla ya ufunguzi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa upande wa Tanzania, miradi 11 imeingia katika mpango huo ambayo inahusu uendelezaji wa sekta ya maji katika mto Songwe, usindikaji wa ngozi, uzalishaji wa mbolea, uchumi wa buluu, nishati, utafiti,, elimu na utengenezaji wa dawa za binadamu na wanyama.

Tanzania imejipanga kutekeleza miradi hiyo hasa ya nishati na uzalishaji wa mbolea ili iweze kuuza katika nchi wanachama ambazo nyingi zinakabiliwa na uhaba wa nishati ya umeme na mbolea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news