NIA KUFIKA SALAMA

NA ADELADIUS MAKWEGA

MACHI 8, 2022 kuna jambo lilinipeleka jijini Dodoma, nilifika katikati ya jiji hilo na kufanya shughuli iliyonipeleka na mpaka saa 9.30 alasiri nilikuwa nimemaliza kazi hiyo na kupanda basi la kurudi Chamwino Ikulu.

Kwa desturi ya Jiji la Dodoma, daladala huwa zinapatikana Kituo cha Sabasaba kwa hiyo nilisogea hadi hapo na kupanda basi hilo lililokuwa Toyota Coaster iliyoonekana mma (mpya).

Tulisafiri na daladala hii mwendo wa dakika 20 tukafika Nanenane, hapo lilisimama kwa kuwa sasa kituoni hapa pana stendi kubwa ya mabasi ya kwenda mikoani na kuna soko kubwa la ndugu yetu Job Ndugai, kwa hiyo kituo hiki kwa sasa huwa na abiria wengi wa safari fupi na hata safari ndefu.

Hapa walipakia abiria wanne, watatu wanaume na mama mmoja. Mama huyu alikuwa mtu mzima, alizungumza na kondakta kwa muda kidogo. Kondakta gafla alisikika akisema.“Mama nauli ni 1000 kama unayo baki ndani ya basi, kana hauna shuka chini.”

Maneno hayo ya kondakta yalitupa picha abiria wote ndani ya basi kuwa mama huyu alikuwa akiomba aheri ya kupunguziwa nauli. Sauti ya kondakta huyu ilikuwa kali mithili ya mwalimu wa nidhamu shuleni na iliweza kuwaamsha abiria kadhaa waliouchapa usingizi wa mchana uliokuwa ukiwanyemelea kana kwamba wamelala katika vitanda vyao majumbani kwao usiku wa manane. Huku wakisituka situka kutokana na kufunga breki kwa basi hili.
“Magana madatu ”
Mama huyu alisema kwa ya sauti ya chini akimanisha shilingi 300/- hana.
Muungwana mmoja mwanaume aling’akha.
“Twendeni Bwana, mimi nitalipa Aisee.”

Kweli jamaa huyu ambaye aliongea kwa matamshi ya kichaga alitoa 500/- na kurudishiwa 200/-
Dereva mwanaume wa daladala hii aliposikia uhakika wa malipo ya kamili ya nauli hiyo ya basi iliyokuwa na usajiri wa T 166 DMU breki ya basi hilo ilikuwa laini mno, aliondoa basi hili tukaendelea na safari kuutafuta Mji wa Serikali-Mtumba.

Nimemtaja dereva mwanaume kwa kuwa sasa wapo madereva wanaume kwa wanawake, Wapo makodakta wanaume kwa wanawake, mambo 50 kwa 50.

Kazi kwetu abiria kuangalia nani bora tu. Nikiwa safarilini niliyarudisha nyuma mawazo yangu juu ya matukio ya zamani wakati wa Ujamaa, kulikuwa na simulizi juu ya madereva, makondakta na wenye magari ya abiria walipokuwa wakituhumiwa kuwashusha abiria misituni kisa hawana nauli.


Huku jambo hili likisababisha abiria kadhaa kuliwa na wanyama wakali wakiwamo Simba, Chui na Fisi na baadhi ya viungo vyao vikikutwa misituni wakati wakitembea kwa miguu kuziokoa nafsi zao misituni.

Kama shauri kama hili la mtu kuliwa na simba sababu ya kushushwa ni kukosa fedha ya nauli kama enzi za uhai wake Marehemu Jaji Raimond Mwaikasu jaji aliyekuwa anathamini uhai wa binadamu katika kuliendesha shauri hilo nina hakika mwendesha mashtaka angekuwa na kazi ya kuwatafuta abiria wote waliopanda basi hilo siku ya tukio hilo alafu wangeeleza kwanini waliacha tukio kama hilo kutokea.

Hakika wangepatikana na kueleza kwanini walishindwa kumsaidia abiria huyu aliyeliwa na Simba msituni.

Hapa nilibaini kuwa kuna wajibu wa abiria kutimiza wajibu wao hata kwa kusema kama kuna jambo baya linafanywa iwe na abiria,utingo, kondakta na hata dereva ndani ya safari ili safari hiyo kuweza kufika salama.

Kukaa kimya ni kulishabikia kosa hilo ambalo baadaye linaweza kuleta madhara kwa mhusika au jamii nzima.

Dereva huyo viwavyo na awe anaweza akaliendesha basi hilo kwa fujo na vurugu kubwa ili aonekane anaweza lakini mwisho wa siku katika kuwakoga wanaomtazama na kumshangilia safari inaweza kufikia pabaya.

Japokuwa katika kusema huku bila shaka unaweza ukaambiwa maneno mengi. “Acha kupiga makelele, kodi taksii kama una fedha nunua gari lako.” Hayo yasikusumbue kumbuka kuwa dereva huyu anaendesha gari hilo kwa leseni ya Serikali, katika barabara ya Serikali (Umma).

Nayeye kama anaweza basi afanye biashara ya kubeba familia yake na ndugu zake na kuwapitisha katika barabara yake na tuone kama hiyo biashara yake itashamiri. Kwa hakika hayo niliyawaza moyoni tu, mara tulifika Buigiri na abiria kadhaa kushuka.

Basi hili liliendelea na safari kidogo mara tuliona moshi ukitoka katika injini. Abiria tulishuka harakaharaka, mara tukisikia Fan belt imechomoka! Mara Rejeta! Dereva na Kondakta wake waliingia uvunguni kuangalia kulikoni?

Tulikaa hapo kwa dakika 7 likaja daladala lengine lenye nambari za usajiri T 109 DUM na sie kupanda gari hilo na kumalizia safari yetu ya Chamwino Ikulu.
Mwanakwetu nia ni kufika salama.
Nakutakia siku njema
makwadeladius@gmail.com0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news