Rais Dkt.Mwinyi:Hatutawafumbiwa macho watumishi wa namna hii

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, haitawafumbia macho watumishi wa umma wasiotaka kuwajibika hasa wanapopelekewa kero za wananchi kuzitatua kwenye taasisi zao na kutozifanyia kazi kwa wakati sahihi.

Hayo yamesemwa leo Machi 29, 2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar, kwenye maadhimisho ya miaka miwili ya mfumo wa Sema Na Rais Mwinyi (SNR).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, mfumo wa SNR umeleta tija kipindi kifupi tokea kuanzishwa kwake, umepokea malalamiko mengi ya wananchi na asilimia kubwa yamepatiwa ufumbuzi kwa watu wengi kupatiwa haki zao na kueleza kwamba Serikali itajitahidi kuondosha kero zaidi za wananchi.

Pia ametoa onyo kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za Serikali wasiotaka kutatua changamoto za wananchi zinazowasilishwa kwenye taasisi zao na kuwaeleza kwamba Serikali itawachukulia hatua.

Rais Dkt. Mwinyi amewaonya baadhi ya watendaji wa taasisi za Serikali wanaowapa vitisho maofisa wao wanaotoa taarifa za ubadhirifu kwenye mfumo wa SNR na kuwaahidi kuwapa ulinzi maofisa wanaotishiwa amani na kuwaeleza wafanye kazi bila woga.

“Asitokee kiongozi yeyote wa Serikali, kuwatisha watoa taarifa kupitia mfumo wa SNR,” ameonya Rais Dkt.Mwinyi.

Aidha, amewaonya baadhi ya maofisa wa mfumo huo kutohoji mamlaka wanapofikishiwa maagizo na kero za jamii, badala yake watekeleze wajibu wao kwa kuzitafutia ufumbuzi unaofaa pamoja na kuwataka watendaji wa serikali kuheshimu na kutii mamlaka za serikali haswa zinapokuja kesi ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali.

“Kama kuna kitu ambacho hakina sababu, wala hatutaki kusikia ni kutokuwajibika kwa maofisa wa SNR kwamba hawatowajibika, Ofisa yoyote wa SNR asietaka kuwajibika, msitegemee Ikulu itachukua hatua, wakuu wa taasisi mko hapa tusije tukalizungumzia tena hapa,”ameonya Rais Dkt.Mwinyi.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, mfumo huo utaendelea kufanya kazi kwa karibu na wanachi na kueleza kwamba mfumo huo una utambuzi wa takwimu kubaini viongozi na taasisi zinazoharibu ama kufanya vizuri hivyo, alieleza wakati umefika kila mmoja aone umuhimu wa kuwajibika.

Akizungumzia suala la taarifa za ubadhirifu wa mali za umma, Dkt. Mwinyi ameahidi kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kiongozi asiyewajibika kwenye majukumu yake.

Rais Dkt. Mwinyi pia amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhuru wa Mahakama, hivyo kupitia mfumo wa SNR Serikali itayafikisha malalamiko ya wananchi kupitia Jaji Mkuu ili yashughulikiwe mahakamani kwa kuondosha kasoro zinazojitokeza.

Ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kutenga bajeti ya kurejesha fidia kwa wananchi na kueleza sasa Serikali itahakikisha inalipa fidia kwa wananchi waliopitiwa na miradi ya maendelo kadri ya wakati ukatavyoruhusu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu, Mhe.Jamal Kassim Ali amesema kuanzishwa kwa mfumo wa SNR ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Nane kwa kuwataka viongozi na watendaji wa ndani ya Serjali wanawajibika kwa vitendo.

Naye Mkuu wa kitengo cha Sema Na Rais, Haji Makame amesema tokea kuanzishwa kwa kitengo hicho miaka miwili iliyopita, kimefanikiwa kupokea changamoto na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa Unguja na Pemba na kuyapatia ufumbuzi kwa baadhi yao.

Amewaeleza mfumo umeziunganisha taasisi 65 za Seriakali na kueleza kwamba una mpango wa kuongeza nyingine zaidi, hivyo aliwaeleza waajiri na wakuu wa taasisi hizo kwamba wanawajibu wa kuwasimamia maofisa wa SNR wanaoshirikiana kufanya kazi kwa pamoja na kitengo hicho na kueleza jukumu la kitengo ni kuratibu majukumu yao.Kitengo cha SNR kipo chini ya Ofisi ya Rais Ikulu, Zanzibar kilianzishwa Februari 27, mwaka 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news