Rais Dkt.Samia atoa pole uvamizi wa kanisa Geita

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Askofu na waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita kwa tukio la kijana wa miaka 25 kudaiwa kuvamia na kuharibu miundombinu ya Kanisa Kuu la jimbo hilo mjini Geita hivi karibuni.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia katika salamu zake alizotuma kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema, Serikali imesitishwa na tukio hilo la kijana huyo (jina linahifadhiwa) kuvamia na kuharibu vyombo, vifaa na maeneo takatifu ya kanisa hilo ikiwemo Altare.

“Rais katuelekeza tuje kutoa pole kwa Askofu, kanisa na waumini wote kwa kilichotokea, bahati nzuri mtuhumiwa amekamatwa, uchunguzi wa utafanyika kubaini kiini na wahusika wote wa tukio hili,”amesema Shigella akiwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt.Samia.

Pia RC Shigella amesema, anaamini huduma katika kanisa hilo liliharibiwa zimesitishwa kwa mujibu wa taratibu za kiimani na kikanisa, na kuahidi kuwa Serikali itashirikiana na uongozi wa kanisa kuona namna ya kuchangia na kuunga mkono kazi ya kurekebisha maeneo yaliyoharibiwa.

Aidha, pamoja na kuharibu mimbari, kijana huyo anayedaiwa kuingia kanisani hapo baada ya kuvunja kioo cha lango kuu pia alivunja kiti cha kiaskofu, misalaba, sanamu za kiimani ikiwemo misalaba na vyombo vya kuhifadhia ya maji ya baraka ambayo pia aliyamwaga.

Tukio hilo linalohesabiwa na waumini na viongozi wa Kanisa Katoliki kuwa sawa na kufuru kwa imani lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia Februari 26, 2023.

Askofu wa Jimbo la Geita, Flavian Kassala ameishukuru Serikali kwa salamu za pole huku akivipongeza vyombo na taasisi za dola kwa kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuanzisha uchunguzi wa kina kubaini kiini na wahusika wote wa tukio hilo alilosema kiimani ni kufuru kwa maeeo takatifu.

“Ni matumaini yetu kama Kanisa na Watanznaia kwa ujumla kuona hatua zilizoanza kuchukuliwa (uchunguzi) zitawafikisha kwenye eneo ambalo jamii wataelewa nini hasa kilikuwa nyuma ya mtuhumiwa wa tukio hili,” amesema Askofu Kassala.

Wakati huo huo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Matindi Kasalla ametoa waraka unaoelekeza kufungwa kwa Kanisa Kuu la Kiaskofu la Jimbo la Geita kwa siku 20 kuanzia tarehe Februari 27 hadi Machi 18, 2013.

Katika waraka wake Askofu Kasalla amesema, uamuzi huo ni kufuatia tukio la kufuru na unajisi lililofanyika ndani ya kanisa hilo ikiwa imefanyika pia kufuru kubwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, na unajisi kwa utakatifu wa jengo hilo la kanisa na vifaa mbalimbali vya Ibada Takatifu.

“Mimi Flavian Matindi Kassala, ambaye kwa Neema ya Mungu na Mamlaka ya Kiti cha Kitume ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, na kwa mamlaka ninayopewa na Sheria Kanuni ya Kanisa (Rejea Na 1211-1213), na kwa maelekezo ya Mamlaka ya Kiaskofu, (Rejea Ceremonial of Bishop namba 1070-1072) napenda kutamka kwamba,

“Uhalifu uliotokea katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita usiku wa kuamkia tarehe 26 Februari 2023 ni kufuru kubwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na umeivunjia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Heshima yake kwa kiasi kikubwa sana na hivyo umeathiri.

"Aidha uhalifu uliotokea katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita usiku wa kuamkia tarehe 26 Februari 2023 umelinajisi kanisa hilo katika utakatifu wake uliowekwa wakati wa Kutabarukiwa kwake,kwani uhalifu uliotokea katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita usiku wa kuamkia tarehe 26 Februari 2023 ni uhalifu mkubwa sana ambao umeiathiri kwa kiasi kikubwa sana hadhi na Muumini Mkatoliki na jamii yetu kwa ujumla,"amesisitiza Askofu huyo.

Askofu Kassala amesema,kutokana na matukio hayo, kanisa hilo limepoteza kwa kiasi kikubwa baraka yake na jamii ya Waamini imeumizwa sana kutokana na Kashfa, Kufuru, na Unajisi uliofanyika kwa Imani.

Na hivyo aliagiza kuwa Kanisa Kuu la Kiaskofu la Jimbo Katoliki la Geita halistahili kwa maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi, wala ya Sakramenti yoyote, wala kwa ibada yoyote.

Hivyo kanisa limefungwa kutoa huduma zote za ibada kwa siku ishirini ilii kwa kipindi hicho kanisa litaingia katika maombi ya toba ya malipizi ikisubiria utakaso ambapo Kanisa limeagiza waumini wote wa jimbo la Geita watafunga huku ikielekezwa mafundisho na mahubiri yote kulenga katika toba na malipizi katika misa mbalimbali.

“Kwa kipindi chote cha kuelekea Toba ya Malipizi waamini wote Wakatoliki wanaalikwa kusali, kufunga, kutubu, kupokea Sakramenti ya Upatanisho na kuomba huruma ya Mungu. Katika Matendo yote haya tuombe Mungu atujalie wongofu wa ndani,”amesema Askofu Kassala.

Amesema, kanisa kuu la jimbo litafunguliwa tarehe 18 Machi 2023 kwa adhimisho ibada ya misa takatifu, na itakayohusisha pia maadhimisho ya toba ya malipizi; baraka kutakatifuza kanisa kuu; na kurudisha ekaristi takatifu ndani ya kanisa kuu.

Aidha, adhimisho la tarehe 18 Machi 2023, litakuwa ni la Kijimbo, na hivyo Mapadre, Watawa, na Waamini wanawajibu wa kuhudhuria.

Watu wote wenye mapenzi mema wanakaribishwa pia kushiriki katika maadhimisho yote haya.

Katika taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Geita limesema uchunguzi umebaini mtuhumiwa aliyefanya uvamizi na uharibifu katika Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Geita ni kijana wa miaka 25 mkazi wa mtaa wa Katundu, Kata ya Kalangalala mjini Geita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi,ACP Safia Jongo amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kueleza jina la mtuhumiwa huyo linaendeleea kuhifadhi kwa sababu za kiusalama.

Amesema, mtuhumiwa amethibitika kufanya uvamizi huo Februari 26, 2023 majira ya saa nane usiku huko katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliyopo mtaa wa jimboni, Kata ya Buhalahala Halmashauri ya Mji wa Geita.

“Baada ya uchunguzi wa awali imeonyesha kwamba mtuhimiwa, kwa nafsi yake ana kitu cha kwake ambacho bado tunaendelea na uchunguzi tujue kwa uhalisia ni nini kilimpelekea kufanya tukio hilo.

“Niombe jamii kutolihusisha tukio hili na kanisa kuwa na mgogoro na taasisi, au kanisa lingine, au dini nyingine, ni mtu mmoja amefanya jambo hili na mpaka sasa uchunguzi unaonyesha ni yeye kama yeye.

“Ukilitazama tukio hili unaona linaambatana na hasira, chuki, visasi, kwa hiyo niombe jamii iondokane na mawazo kama hayo, kama una jambo dhidi ya mtu basi fuata taratibu za kisheria, au za kijamii."

Alithibitisha vilivyoharibiwa ni Tebernakulo na taa yake, kipaza sauti, stendi za mishumaa, kitabu cha masomo ya misa, nguo na vitambaa, mito ya viti vya askofu, msalaba wa maandamano, sanamu ya bikra Maria, diaba la maji ya Baraka.

Aliongeza, pia vioo vya mlango mkuu, vioo vya madirisha, kiti cha maungamo, kinawa cha mishumaa, kioo cha sakristia, control boksi ya CCTV kamera, kamera ya sakristia, choo na feni na thamani ya vitu vyote haijajulikana.

“Mtuhumiwa kabla ya kutekeleza uharibifu huo Februari 25, 2023 majira ya saa mbili usiku alikwenda kunywa pombe katika baa iitwayo Meeting Point, iliyopo mtaa wa Kalangalala mjini Geita akiwa na mwenzake,"amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news