Rais Dkt.Samia azidisha mashangilio nchini

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema hakuna sura za kushika dola kutoka upinzani na kwamba mwaka 2025 yeye yupo na badala ya kusema 'Mwamba Tuvushe' waseme 'Mama Tuvushe'.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Maridhiano kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe aliyeikabidhi kwa niaba ya Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA). (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Machi 8, 2023 wakati akishiriki Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lilioandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) katika Ukumbi wa Kuringe mkoani Kilimanjaro.

Wakati akiwasili ukumbini hapo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alipokelewa na viongozi mbalimbali wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa chama Taifa,Mheshimiwa Freeman Mbowe. 

Pia mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa Kamati Kuu ya CHADEMA, viongozi wa kanda na mabaraza, Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,wabunge, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, viongozi wa dini,wanachama na wageni wengine waalikwa.

“Kwa sura ninazoziona hapa hamna dhamira ya kushika dola 2025 mnajua mama yupo, dhamira hiyo haipo. Wote mfanye siasa za kistarabu, katika kipindi kifupi nchi yetu inaheshimika duniani tusiirudishe nyuma, Tanzania ni taifa kubwa tusilitolee sifa yake.

“Najua wakati nilipopendekeza kwenye chama changu tufungue mikutano wa hadhara mjadala ulikuwa ni mkubwa, haikuwa rahisi, najua juzi Mbowe (Freeman) alikuwa na mjadala mkubwa sana kwa nini umemuita Rais kwenye mkutano wetu, kwa hiyo wahafidhina wapo wengi, kwenye chama chako, chama chetu.

“Najua unatandikwa umepewa asali umebadili na ‘tone’, ulipotoka jela ulienda Ikulu mama alikwambia nini? Ukienda nje unatandikwa…wahafidhina siku watatuelewa, asante ndugu yangu (Mbowe).

“Leo hapa tumejawa na furaha, na hiyo ni sababu ya matunda ya mazungumzo ya maridhiano ndugu zangu siasa ni mchezo wa kulumbana kwa hoja,kasema nini nimzodoe, wote tukiwa na lengo la kushika dola.

“Mimi Dada yenu (Mheshimiwa Rais Samia) na wenzangu wanaonisaidia tumefanya ubunifu wa kuhakikisha Taifa hili linaungana na kuwa moja. Tukaviambia vyama vya siasa vikae na kuja na namna wanataka tufanye nini.

“Katika hilo chama chenu kikaja na maoni yake ya kutaka kisikilizwe peke yake na mimi nikamwambia Makamu wangu awaite watu wenu watano na upande huu watano mambo yakasonga mbele.

"Baada ya vikao hivyo leo mnamuona Rais amesimama kwenye jukwaa hili kuzungumza na Baraza la Wanawake la CHADEMA, jambo ambalo halikuwa rahisi huko nyuma ila kwa sababu ya ubunifu limewezekana,”amefafanua kwa kina Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Malezi

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amewataka wazazi kuangalia sehemu waliyokosea kwenye suala la malezi ya watoto na kulifanyia kazi suala hilo ikiwemo kuzingatia mila na desturi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili nchini.
“Kuna mengine ya kuletewa tukatae yale ya kuletewa, sisi kama taifa tukatae yale yakuletewa, kwa sababu yakija hayamuumizi mmoja, leo yamemuumiza jirani kesho yataingia kwako,”ameagiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameshauri wazazi kuhakikisha watoto wao wanawapa mafunzo ya dini ili kuepukana na mmomonyoko huo wa maadili katika jamii na Taifa.

Wakati huo huo ameshauri viongozi wa dini, serikali kuungana kwa pamoja na kuona nini cha kufanya katika kulinda maadili ikiwemo kuzilinda mila na desturi.

Katiba je?

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, hivi karibuni ataunda kamati kwa kushirikiana na vyama vingine vya siasa ambayo itashughulika na suala la katiba mpya nchini.

“Suala katiba hakuna anayekataa hata chama changu hakuna anayekataa, na muda si mrefu tutatangaza kamati ambayo itashughulikia jambo hilo.Hakuna kisichowezekana kwa mazungumzo, tulishuhudia nchi kadhaa ziliingia kwenye vita hakukupatikana suluhu, lakini suluhu ikaja kupatikana kwa mazungumzo,"amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia akizungumzia kuhusu suala la wabunge 19 wa CHADEMA, amesema kuwa Mahakama iachwe ifanye kazi yake kwa kuwa hata kama yeye ni Rais bado hana mamlaka ya kugusa huko.

Rais Dkt.Samia ameshukuru kwa kualikwa kwenye mkutano huo wenye lengo la kuwathamini na kuwapa haki wanawake wa Tanzania na duniani kote. 

“Huwezi kuitwa na wananchi wako ukasema...siji, nilifurahi kuja kwa kuwa nitasikia CHADEMA wanasema nini, na nimesikia wanawake wa CHADEMA na CHADEMA kama chama kinasema nini.

“Wanasema haijapata kutokea, kwangu mimi ni faraja na leo tunaandika historia mpya ya kuendelea kuliunganisha taifa letu,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Mwenyekiti Mbowe

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe amewashukuru wanawake wa BAWACHA pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki mkutano huo wenye lengo la kuimarisha umoja na mshikamano kama taifa.
Mheshimiwa Mbowe amesema,wanawake wa CHADEMA kama walivyo wanaume wa chama hicho hubaguliwa na kupitia maumivu mengi kwa sababu za kichama. 

Pia amekumbusha kuwa baada ya kualikwa Ikulu siku ya kwanza alipotoka jela walisisitiza haki kwa kuwa huliinua taifa na pasipo haki, Taifa hulaanika. 

Amemshukuru Rais kwa kuyapa nafasi maridhiano pamoja na kuonesha nia ya kuthubutu katika kurejesha haki na kuondoa mpasuko wa kitaifa uliokuwepo.

Suala la watu kujiita chawa wa mama, Mheshimiwa Mbowe amesema, "Unafiki na uongo hulaanisha taifa. Taifa letu lina watu wengi wasio sema na kuuishi ukweli. Hili ni chimbuko kubwa la mporomoko wa maadili. Nakusihi sana mama, epuka mtu yeyote anayejiita chawa wako,"amesema Mbowe.

Mheshimiwa Mbowe amesema, amechagua kusema ukweli na kukataa dhambi ya unafiki, huku akisisitiza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa makini na watu hao wanaojiita chawa wake.

Mheshimiwa Mbowe amesema, wamelipa gharama kubwa kwa misingi na misimamo hiyo. Amesema, wao CHADEMA wanaamini katika ukweli, uwazi, kutokuwa wanafiki ndiyo njia bora ya kusaidia kusonga mbele.

“Hatutokuwa wanafiki ili uweze kuwa kiongozi bora, tutasema ukweli ndiyo njia bora ya kuisaidia serikali iweze kutekeleza wajibu wake.

“Sisi kama chama kikuu cha upinzani tutaishi maisha hayo bila woga wowote, bila unafiki, bila kujikomba bila uchawa tutanyoosha na tutasema kama inavyostahiki.

“Kwa sababu tunaamini hiyo ndiyo njia sahihi ya kuwatengenezea watoto na watoto wa watoto wetu Taifa bora siku zijazo kwa kizazi kijacho. Hofu hizi lazima tuzimalize kwa vitendo, ukiwa mkuu wa nchi ukawa mkatili, mfumo mzima wa utawala wako unakuwa katili.

“Ni matumaini yangu, Mheshimiwa Rais, azma yako ya kuliweka Taifa pamoja itarithiwa na viongozi waliopo chini yako, waliopo katika serikali yako, waliopo katika taasisi mbalimbali za utoaji haki katika Bunge, Mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama na watu wote wanaoshika katika utawala na uongozi wa watu,”amesema Mheshimiwa Mbowe.

Mheshimiwa Mnyika

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika ametoa mapendekezo ya kuikumbusha serikali pamoja na vyama vyote vya kisiasa kuwa kila jambo wanalofanya liwe linazingatia maslahi na makatwa ya wananchi kwa kuwa hii ni nchi yao. 
Mheshimiwa Myika amesema, nchi ni ya wananchi, lazima wakati wote vyama vikuu visikilize wananchi na kwenda pamoja kutekeleza matakwa ya Watanzania

“Watanzania wanalilia...hali ngumu ya maisha na katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Mambo haya kwa safari mliyoianza kuanzia Mwenyekiti Mbowe (Freeman) alipotoka gerezani ya kuliunganisha Taifa katika haki na safari ya mwaka mzima mliyoenda nayo kwa njia mbalimbali. Ninaamini safari hii ikiendelea mbele kwa pamoja kama Watanzania hakika tutafika katika nchi tunayoitafuta,”amesema Mheshimiwa Mnyika.

RC Babu

Nurdin Babu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuongoza Watanzania hasa wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao umepelekewa shilingi bilioni 217 kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake kwa ajili ya maendeleo.

“Tumeletewa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali shilingi bilioni 217 na zimeenda sekta ya elimu, afya, barabara, maji, kilimo. utalii na uwezeshaji wananchi na ushirika,”amesema.

Mheshimiwa Babu amesema, sekta ya afya peke yake imepelekewa shilingi bilioni 42.5 na zimefanya kazi kubwa.“Na jana tumeletewa shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kumalizia jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Mawenzi,”amesema.

Pia amesema, Sekta ya Elimu,walipelekewa shilingi bilioni 21 ambazo wamejenga shule mpya za sekondari tisa na walipelekewa shilingi bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Aidha,kwa upande wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro,RC Babu amesema mkoa huo umepelekewa shilingi bilioni 53 na jana wamepelewa shilingi bilioni 12.5 kwa ajili ya kukarabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. 
Mheshimiwa Babu amesema, kwa upande wa maji, zimepelekwa shilingi bilioni 14 na miradi inaendelea, kilimo utalii na mazingira nako wanajitaidi kwa kuhakikisha wanapanda miti ya kutosha.

Akizungumzia kilimo amesema, zimepelekwa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya mbolea ya ruzuku na mkoa huo umepewa pikipiki 245 kwa ajili ya maofisa ugani kwa ajili ya kuendelea shughuli za kilimo na mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu inazidi kutolewa kwa kasi.

Mwenyekiti BAVICHA 

Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa, Sharifa Sulleman ametaja mafaniko kadhaa yaliyochangiwa na BAWACHA kichama na katika ngazi ya Taifa.

Aidha,ameelezea mambo waliyofanyiwa wanawake kwenye chaguzi za mwaka 2019 na 2020 ambao amesema ulikuwa ni unyanyasaji mkubwa uliofanywa kidikteta.

Pia amemuomba Rais Dkt.Samia kupunguza bei za vyakula na kudhibiti mfumuko wa bei,kuongeza kima cha chini cha mshahara,kuboresha sekta ya afya na kurejesha mchakato wa Katiba na tume huru ya uchaguzi.
Wakati huo huo amemuomba Rais Dkt.Samia kuangalia kwa jicho la tatu kesi inayowakabili wabunge 19 wa chama hicho na kulipatia majibu. 

Mwenyekiti huyo amewakaribisha wanachama waliokimbia nchi na kuwataka wajisikie kuwa wapo nyumbani na kuwahakikishia kuwa zama za kutekana na kupotezana hazina nafasi kwa sasa katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia.

BAVICHA Kilimanjaro

Grace Kiwelu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) Mkoa wa Kilimanjaro na mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ameeleza mbele ya Rais Dkt.Samia namna viongozi wa baraza hilo la wanawake walivyodhalilishwa na kukataliwa kuotesha miche ya matunda katika Shule ya Sekondari Kiboriloni iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani humo.

Mwenyekiti huyo amemweleza Rais Dkt.Samia kuwa, Machi 3, mwaka huu walienda shuleni hapo kwa lengo la kuotesha miche ya matunda, lakini walikataliwa na mmoja wa watumishi wa shule hiyo kwa kile alichoeleza kuwa mtumishi huyo aliwaeleza kuwa hawawezi kuotesha miche hiyo kwa kuwa wao siyo chama tawala.

"Mheshimiwa Rais tunakupa heko kwa kulinda maadili katika nchi yetu, Mkoa wetu wa Kilimanjaro ni kati ya mikoa ambayo ina joto kali sana, sisi wanawake wa CHADEMA tuliamua kufanya zoezi la kupanda miti ya matunda na vivuli ndani ya mkoa wetu.
"Tulifuata taratibu zote za maandalizi ambapo siku ya Ijumaa tulipanda miti katika Zahanati ya Merybenet katika Halmashauri ya Moshi DC, ingawa zoezi hili lilitanguliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo na hatimaye lilifanikiwa baada ya uongozi wa serikali kuingilia kati na kutoa maelekezo.

"Mheshimiwa Rais, tulipofika Moshi tulikutana na upinzani mkubwa katika Shule ya Sekondari kiboriloni, tulifanyiwa unyanyasaji, tulinyimwa kuotesha miti Ile ambayo tulinunua kwa fedha zetu kutoka mifukoni mwetu.

"Mmoja kati ya watumishi wa shule Ile alitukatalia kwamba haturuhusiwi kuotesha miti Ile maana sisi siyo chama tawala, baada ya kupambana alisema hata yeye analinda ugali wake,kwa masikitiko makubwa tulilazimika kuondoka na miti yetu,"amefafanua Mwenyekiti huyo wa BAWACHA mkoani Kilimanjaro.

Katibu BAWACHA

Wakati huo huo Katibu wa BAWACHA Taifa, Carherine Ruge amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kukubali kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo na amesema kuwa hawakumualika Rais kimakosa, kwani ni mwanamke mwenzao na kiongozi wa Taifa.

Pia,amejivunia kujenga baraza imara lenye ushawishi mkubwa nchini, amemkumbusha Rais Dkt.Samia kuwa, wanawake ni jeshi kubwa na wapo milioni 31 kwa mujibu wa Sensa iliyopita. 

Aidha, amesema, pamoja na wingi huo, hadhi ya wanawake nchini ni ndogo, wanaishi maisha duni na kwenye mkutano huo pekee, wanawake 3234 walihudhuria.

Ruge amemshauri Rais Dkt. Samia kutokuogopa kukatishwa tamaa na wale wasioitakia mema nchi hii ambao kwa kiasi kikubwa ni wanaume, kwani mwanamke akiamua jambo lake hulifanya pasipo kurudi nyuma.

BAWACHA imetambua juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia akishirikiana na Mhe. Freeman Mbowe katika maridhiano na kutafuta katiba mpya kabla ya mwaka 2025. Ameomba jambo hilo liendelee kufanyika kwa kasi kubwa ili matamanio ya watu yaweze kutimia.
Amesema, pamoja na mazuri yanayoyafanywa na Rais Samia, kupitia kongamano hilo atafungua sikio na kusikia yale ambayo wanawake wenzao wa CCM hawamuambii.“Yale ambayo yanahitaji utashi wako ambayo haujayasikia, utayasikia,"amesema Ruge.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka huu ni "Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news