Rais Dkt.Samia:Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia kuleta mageuzi ya kilimo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wadau wa kilimo kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na wataalam wa kilimo kubuni mipango ya maendeleo itakayoleta mageuzi katika sekta hii.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi mfano wa Funguo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya umwagiliaji Raymond Mndolwa kwa ajili ya Programu ya Kilimo cha Mashamba Makubwa ya pamoja (Block Farming) Chinangali mkoani Dodoma Machi 20, 2023.

Rais Samia ametoa wito huo Machi 20, 2023 kwenye uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja (block farming); utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji; na kukabidhi mitambo na magari kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliyofanyika Chinangali, wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Aidha, Rais Dkt.Samia amesema uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana na wanawake kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo bora (Building a Better Tomorrow - BBT).

Vile vile, Rais Dkt.Samia amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejidhatiti kuhakikisha mpango huu unakuwa endelevu na unafikia mafanikio yaliyokusudiwa.

Pia amesema miongoni mwa malengo ya Serikali kwa upande wa kilimo cha mazao, uvuvi na ufugaji ni kuwa na kasi ya ukuaji wa sekta kufikia 10% katika pato la taifa ifikapo mwaka 2030 kutoka 3.6% ya hivi sasa.

Rais Dkt.Samia amemtaka Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kuhakikisha anasimamia kikamilifu fedha zote zinazotolewa katika mradi huo ili iweze kuzalisha bila kufanyiwa ubadhirifu.

Utekelezaji wa Mpango wa Mashamba Makubwa ya Pamoja kupitia BBT umeanzia mkoa wa Dodoma katika Shamba la Chinangali II lenye ekari 400. Hekta zaidi ya 47,000 zimeshapatikana katika mikoa mingine na upimaji udongo unaendelea ili kutambua mahitaji ya virutubisho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news