Serikali yajivunia uthabiti Sera ya Fedha

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Fedha na Mipango,Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, kupitia uratibu madhubuti wa Sera ya Fedha, Tanzania imeweza kutekeleza sera na uendeshaji ambao umeokoa uchumi wa nchi kutokana na mtikisiko wa kidunia hivi karibuni.
Hayo ameyasema leo Machi 3, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mhadhara wa 8 wa Kumbukumbu ya Gilman Rutihinda ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 
Mhadhara wa Kumbukumbu ya Gilman Rutihinda ulizinduliwa mwaka 1995 kwa heshima ya marehemu Gilman Rutihinda, Gavana wa tatu wa Benki Kuu ya Tanzania, kutokana na mchango wake mkubwa katika sera za uchumi na maendeleo. Bw.Rutihinda alifariki Juni mwaka 1993 akiwa bado Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Aidha, Waziri Dkt.Nchemba ametaja ukuaji wa uchumi wa asilimia 4.9 mwaka 2021, wastani wa ukuaji wa asilimia 5.2 katika robo tatu ya kwanza ya mwaka 2022 na mfumuko wa bei ulioongezeka kidogo hadi asilimia 4.9 hivi karibuni kutokana na uratibu madhubuti wa Sera ya Fedha.

“Niwahakikishie kwamba binafsi, mimi ni mtetezi mkubwa wa uratibu katika maeneo haya na mengine. Na, kwa Wizara ya Fedha na Mipango, ningependa kuthibitisha ahadi yetu ya muda mrefu katika kudumisha uratibu wa Sera Fedha,"amesema.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania,Sera ya Fedha ina jukumu la kuhakikisha ujazi wa fedha katika uchumi wa nchi unawiana na malengo ya utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi. 
Dkt.Nchemba amesema, mwenendo wa sasa duniani unafanya uratibu wa sera kuwa muhimu zaidi katika kuendeleza ukuaji wa uchumi na ustawi wa watu.

Kauli mbiu ya mhadhara wa mwaka huu ilikuwa ‘Kuimarisha Uratibu wa Sera ya Fedha katika kukabiliana na Changamoto za Kiuchumi Duniani’ huku mgeni rasmi akiwa ni Prof. Shantayanan Devaran, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Georgetown, Marekani.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Dkt.Patrick Njoroge aliongoza kikao hicho huku Prof.Jehovahness Aikaeli kutoka Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Usimamizi wa Uchumi na Usimamizi wa Fedha Mashariki na Kusini mwa Afrika (MEFMI) wakichokoza mada.
Akiwakaribisha washiriki wa mhadhara huo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania alisisitiza umuhimu wa uratibu wa sera ya fedha akisema kufanya hivyo ni muhimu katika kuhakikisha utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi.

Waliohudhuria katika mhadhara huo ni mjane wa marehemu Rutihinda, Bi.Josephine Rutihinda, watoto wake watatu na ndugu wengine, Manaibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Wajumbe wa Bodi ya Benki Kuu ya Tanzania.
 
Muhimu
 
Mbali na hayo, Benki Kuu ya Tanzania hutumia nyenzo mbalimbali  kutekeleza Sera ya Fedha  ambazo ni uuzaji na ununuzi wa  dhamana (debt securities), uuzaji na ununuzi wa fedha za kigeni  kutoka soko la  fedha za kigeni baina ya mabenki, nyenzo za repo and reverse repo, mikopo kwa mabenki ya biashara na kiasi cha amana za benki  za biashara kinachotakiwa kuwa Benki Kuu (Statutory Minimum Reserve) na huduma za muda mfupi za ukwasi kwa mabenki (intraday and Lombard loan facilities).

Aidha,Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikihakikisha uwazi katika uundaji na utekelezaji wa Sera ya Fedha. 

Maamuzi ya Kamati ya Sera ya Fedha (Monetary Policy Committee) kuhusu sera ya fedha iliyoamuliwa huwasilishwa kwenye mkutano na wakuu  wa benki za biashara na pia huwasilishwa kwa umma kupitia vyombo vya habari. 

Pia, Benki Kuu huchapisha ripoti za vipindi mabalimbali zinazoonesha sera ya fedha iliyopo, utekelezaji wake na muelekeo wa uchumi wa Tanzania kwa ujumla. Ripoti hizo huwekwa pia kwenye tovuti ya Benki Kuu www.bot.go.tz

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news