SERIKALI YASHAURIWA UMUHIMU WA KUANZISHA BARABARA ZA KULIPIA TOZO

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuanza na mfumo wa barabara zenye tozo katika mradi wa ujenzi wa barabara njia nane kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha Mkoa wa Pwani ili kuweza kuongeza mapato.
Ushauri huo umetolewa wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara kutembelea mradi wa barabara wa njia nane ambapo waliongozana na viongozi na watumishi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuona maendeleo ya mradi huo ulipofikia pamoja na kuona changamoto zilizopo.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuduma ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso amesema, duniani kote, barabara nyingi zinajengwa kwa mfumo kama wetu ambao ulishaanza muda mrefu na sheria inatukataza huwezi kuwa na barabara ya tozo kama huna njia nyingine mbadala.
Aidha,amesema katika mradi wa barabara kunatakiwa pia kuimarishwa kwa mifumo ya mifereji kwa ajili ya majitaka kwani mvua zinaponyesha maji yanashindwa kwenda kwenye maeneo husika na kuleta kero kwa watumiaji wa barabara.

Pamoja na hayo, Kamati hiyo imeridhishwa na miundombinu inayojengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuipongeza Wizara kwa usmamizi mzuri ambao wanaufanya kupitia TANROADS kujenga miundombinu ya barabara nchini.

"Tumeiona dhamira ya Serikali kupunguza msongamano ambao wanaamini utarahisisha shughuli nzima kwenye sekta ya uchukuzi,"amesema Mhe.Kakoso.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kumekuwa na ongezeko la gharama kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu kutoka kwenye gharama ya mwanzo mpaka mradi unapokaribia kuisha, gharama zinaongezeka kutokana na usanifu wa ujenzi wa miundombinu mipya.

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema mradi huo uliogharimu shilingi za kitanzania bilioni 218 umejengwa na Mkandarasi mzawa kutoka kampuni ya ESTIM CONSTRUCTION umefikia asilimia 98 na unatarajia kukamilika mwezi ujao.

Mhandisi Mativila amesema, watahakikisha wanayasimamia kikamilifu maelekezo na ushauri ili kufikia matarajio yanayokusudiwa hasa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news