SHULE KWA WAHAFIDHINA: Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika

NA LWAGA MWAMBANDE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema,kazi ya maridhiano sio rahisi kwa pande zote mbili kwa maana ya chama tawala na upinzani.

Amesema,alipopendekeza kuruhusu mikutano ya hadhara kulikuwa na ugumu kwenye chama chake kama ambavyo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe anavyopitia magumu kwenye chama chake ikiwemo kuambiwa amelamba asali.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Machi 8, 2023 wakati akishiriki Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lilioandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) katika Ukumbi wa Kuringe mkoani Kilimanjaro.

“Mageuzi yapo na tutajenga Taifa jipya, tutajenga Taifa la Tanzania lenye ushindani wa kisiasa sio wa vurugu, nilipopendekeza kwenye chama changu tufungue mikutano ya hadhara kulikuwa kugumu kidogo, mjadala ulikuwa mkubwa kidogo kama mnavyofanya nyie.

“Najua juzi Mbowe alikuwa na mjadala mkubwa kidogo, kwa nini mmemuita Rais kwenye hili jukwaa? Kwa hiyo Mwenyekiti Mbowe wale Wahafidhina wapo kwako wapo na kwangu pia.

“Wapo waliomwambia Mbowe ushalishwa asali, tuambie Ikulu siku uliyotolewa jela umwekwenda kuambiwa nini? Mbona umekuja na tone hii sasa hivi? Akienda nje anatandikwa anawaambia jamani sitaki kurudi kule, mwendo ni huu kama tunavyokwenda asante sana ndugu yangu Mbowe hapo hapo, Wahafidhina watatuelewa jinsi matokeo yanavyotokea, lengo kubwa kujenga amani na utulivu tupate maendeleo.

“Leo hapa tumejawa na furaha, na hiyo ni sababu ya matunda ya mazungumzo ya maridhiano ndugu zangu siasa ni mchezo wa kulumbana kwa hoja,kasema nini nimzodoe, wote tukiwa na lengo la kushika dola.

“Mimi Dada yenu (Mheshimiwa Rais Samia) na wenzangu wanaonisaidia tumefanya ubunifu wa kuhakikisha Taifa hili linaungana na kuwa moja. Tukaviambia vyama vya siasa vikae na kuja na namna wanataka tufanye nini.

“Katika hilo chama chenu kikaja na maoni yake ya kutaka kisikilizwe peke yake na mimi nikamwambia Makamu wangu awaite watu wenu watano na upande huu watano mambo yakasonga mbele.

"Baada ya vikao hivyo leo mnamuona Rais amesimama kwenye jukwaa hili kuzungumza na Baraza la Wanawake la CHADEMA, jambo ambalo halikuwa rahisi huko nyuma ila kwa sababu ya ubunifu limewezekana,”amefafanua kwa kina Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Pia mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa Kamati Kuu ya CHADEMA, viongozi wa kanda na mabaraza, Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,wabunge, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, viongozi wa dini,wanachama na wageni wengine waalikwa.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia, Mwenyenzi Mungu amemkiria karama ya kipekee katika uongozi ambayo imejikita zaidi katika kupatanisha, kuunganisha wananchi wa itikadi zote kwa ustawi na uendelevu wa Taifa letu. Endelea;


1.Shule kwa wahafidhina, maisha ni kupatana,
Na wala si kuzilana, kutakiana laana,
Kila siku kuumana, kwa kucha kuparurana,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

2.Taifa tunaliona, jinsi vidonda vyapona,
Kule kote kusigana, glasi wagongeana,
Mwisho sote tutanona, mema tukizidi vuna,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

3.Kiongozi twamuona, mapokeo ayachana,
Kwa sasa yameshachina, hakuna kuchuniana,
Siasa tutaziona, ni za hoja kupambana,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

4.Jana nani aliona, Rais anakutana,
Kwenye siku kubwa sana, na Chadema akutana,
Mawazo badilishana, kwake hawajamuona,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

5.Ni ukomavu twaona, tena tunafundishana,
Wavulana wasichana, kuchukiana hakuna,
Tufanye ya kujengana, kwa Amani ni amana,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

6.Wale walitishiana, na vikumbo kupigana,
Sasa pamoja twaona, kwa hoja wanashindana,
Tena wasalimiana, bila dharauliana,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

7.Kesho kama twaiona, jinsi tutatulizana,
Chaguzi tukiziona, vijiti badilishana,
Akipata tukiona, mbele tutaelewana,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

8.Wenye macho wanaona, unaingia mchana,
Ila kwa wasioona, meno yao yasigana,
Pole kwa wahafidhina, yajayo mnayaona,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

9.Nchi hatutagawana, yetu sote tunaona,
Tutazidi kushindana, pasi hata kupigana,
Kisha tutatulizana, kwa pamoja kujichana,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

10.Samia tunakuona, unazidi kutukuna,
Waupiga mwingi sana, mema mengi unavuna,
Mwanga mwingi twauona, mema tutazidi ona,
Huu ukurasa mpya, siasa yabadilika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news