Tanzania yakabidhi misaada ya kibinadamu kwa Serikali ya Malawi

NA MWANDISHI WETUHABARI

BALOZI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Humphrey Polepole ameshiriki katIka zoezi la kukabidhi misaada ya kibinadamu kutoka Tanzania kwa Serikali ya Malawi ili kusaidia waathirika wa Kimbunga Freddy. 
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi, Mhe.Humphrey Polepole akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Nancy Tembo misaada ya kibinadamu iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi amekabidhi misaada hiyo ya kibinadamu inayojumuisha mablanketi, mahema, unga wa mahindi leo Machi 25, 2023 kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Nancy Tembo katika Mji wa Blantyre nchini Malawi.

Balozi Polepole amebainisha kuwa, wa Watanzania, na watu wa Malawi ni jamii moja, na nia ni kuendekeza umoja uliojengwa na waasisi wa nchi zetu. 

"Msaada huu wa kibinadamu utasaidia, katika jitihada za kurejesha matumaini na ustawi kwa ndugu zetu wananchi wa Malawi,"amesisitiza Balozi Polepole. 

Ameongeza kuwa, ana imani na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioenda nchini Malawi watashirikiana na wenzao wanajeshi wa Malawi, kuhakikisha kwamba misaada iliyotolewa inawafikia waathirika wa Kimbunga Freddy. 
Waziri wa Mambo ya Nje nchini Malawi, Mhe. Nancy Tembo akimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Humphrey Polepole wakati wa kukabidhiwa misaada kwa waathirika wa Kimbunga Freddy. 

Aidha, Tanzania imetoa madawa ya binadamu, ambayo yataweza kusaidia kwenye maeneo ambayo vituo vya afya vimeathirika. Hizi zote ni jitihada za kusaidia nchi ya Malawi katika kurejesha huduma za afya.

"Tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada aliotoa kwa nchi ya Malawi, kwa uwezeshaji wa fedha na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Wahandisi wa Medani) ambao watasaidia katika kurejesha hali ya miundombinu nchini Malawi,"amesema Balozi. 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi ya Malawi Mhe. Nancy Tembo ameshukuru nchi ya Tanzania kwa msaada wa kibinadamu iliowapatia, ambao umefika katika wakati muafaka. 
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Humphrey Polepole akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo, Watendaji idara ya Menejimenti ya Mafaa ya Tanzania na Malawi na Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania watakao shiriki katika Operesheni kusaidia Wahanga wa Kimbunga Freddy. 

“Msaada huu ni muhimu kwetu kwa sababu tunao Wanachi wengi ambao makazi yao yameharibika, na tunahitaji msaada wa kila mtu ili kuhakikisha wahanga wa Kimbunga Freddy wanapatiwa huduma za msingi kwa wakati,”amesema Waziri Nancy. 

Ameongeza kuwa, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wamekuja kuwasaidia na wataungana na askari wa NchinMalawi katika kurudisha miundo mbinu iliyoharibika katika hali ya kawaida. 

“Nachukua fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutusaidia katika wakati ambao tunahitaji msaada sana, janga hili ambalo limeathiri Nchi ya Malawi, limegharimu maisha ya watu, na limeharibu miundo mbinu” alisema Waziri Nancy. 

Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulika na Operesheni pamoja na Uratibu wa shughuli za Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu, Luteni Kanali Selestine Masalamado ametoa pole kwa wananchi wa Malawi kwa maafa ya Kimbunga Freddy. 
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Humphrey Polepole akiwa na Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania watakaoshiriki katika Operesheni kusaidia waathirika wa Kimbunga Freddy. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa kuratibu suala la misaada ya kibinadamu kwa ajili ya waathirika wa Kimbunga Freddy nchini Malawi, ambapo kwa awamu ya kwanza helikopta mbili kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania zilisafiri kuja Malawi kufanya kazi za wokozi, lakini msaada wa pili ilikuwa ni msaada wa fedha kwa Serikali ya Malawi na tatu ni kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika wa Kimbunga Freddy.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news