TUSITISHANETISHANE:Hakuna Taifa,nchi iliyo bora kuliko nyingine

NA LWAGA MWAMBANDE

"Jumuiya ya Kimataifa inatambua kwamba hakuna nchi iliyo bora kuliko nyingine, hakuna mfano wa utawala ambao ni wa ulimwengu wote, na hakuna nchi moja ambayo inapaswa kuamuru utaratibu wa kimataifa," aliandika Rais wa China, Xi Jinping katika op-ed (nathari) iliyochapishwa katika vyombo vya habari vya China na Urusi baada ya kutembelea Moscow.

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping nchini Urusi wiki hii, ambayo pia ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuchaguliwa tena kuwa rais wa China, inaaminika kuwa safari ya urafiki, ushirikiano na amani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Xinhua, mbali na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili, Xi na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, walijadili masuala yanayotikisa duniani, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa Ukraine, na kufikia makubaliano.

Viongozi hao wawili walitia saini na kutoa taarifa ya pamoja na kusisitiza haja ya kutatua mgogoro wa Ukraine kwa njia ya mazungumzo. Upande wa Urusi unasisitiza dhamira yake ya kuanza tena mazungumzo ya amani haraka iwezekanavyo.

Pia, katika kikao na waandishi Rais Putin akiwa na Xi huko Kremlin, Xi alisema China wakati wote imekuwa ikihimiza mazungumzo ya amani juu ya mzozo wa Ukraine.

Huu ni mwendelezo wa juhudi za China kuchukua jukumu kubwa katika kuleta amani baada ya kufanikiwa kusuluhisha na kuleta maelewano kati ya Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislam ya Iran.

Machi 10, nchi hizo mbili za Mashariki ya Kati zilifikia makubaliano huko Beijing kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.China imekuwa ikiamini zaidi katika kudumisha umoja, mshikamano, amani na kudumisha utu wa binadamu popote pale duniani. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ifahamike na ndivyo ilivyo kuwa, Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane. Endelea;


1.Haya ni maneno kuntu, wanayasikia huko?
Tena yasemwa na mtu, naye ana nguvu huko,
Ni kiongozi wa watu, tena wengi sana huko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

2.Kwa sababu tunao watu, wanajitangaza huko,
Ya kwamba wao ni watu, hata wafanya vituko,
Kwamba wengine vijitu, hatuonekani huko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

3.Sasa ni kipimo chetu, yanayotokea huko,
Vipi watafanya kitu, au waufyata huko,
Sababu twaona watu, wenye nguvu wako huko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

4.Tena watu wako fyatu, silaha wanazo huko,
Jaribu utende kitu, umwage ugali huko,
Hakuna salama katu, mboga watamwaga huko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

5.Maneno ya roho kwatu, hebu sikizeni huko,
Mtuache sisi watu, tukiishi na kicheko,
Vurugu zenu ni kutu, zatesa huku na huko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

6.Dunia inao watu, wanajijua waliko,
Wajiona wao watu, wa kuishi na kicheko,
Na wengine siyo watu, yawakute hukohuko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

7.Sasa waibuka watu, wawatisha hata huko,
Yalopita siyo kitu, ya sasa hatari huko,
Kichwakichwa ukurutu, watatoka nao huko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

8:Tunawahitaji watu, wenye kukemea huko,
Kwa vile sauti zetu, wengi hazifiki huko,
Ingawa mapenzi yetu, Amani huku na huko,
Dunia ni yetu sote, tusitishanetishane.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news