Waziri Mkuu azindua mifumo ya kibiashara ya JIBA

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua programu ya kompyuta maarufu kama JIBA App iliyotengenezwa na taasisi ya kibiashara ya Jaffery International Business Association (JIBA) tawi la Tanzania. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Taasisi ya Usaidizi na Uhusiano wa Kibiashara (JIBA) kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam, Machi 12, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Programu hiyo ambayo lengo lake kuu ni kutengeneza fursa za biashara, itawezesha upatikanaji wa taarifa juu ya fursa za uwekezaji za ndani na nje ya nchi na hivyo kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wanachama wa JIBA ambao ni wafanyabiashara wakubwa na wadogo. 

Akizungumza na washiriki kwenye hafla ya uzinduzi iliyofanyika jana usiku wa Machi 12, 2023 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema programu hiyo inatarajiwa kupunguza usumbufu na kuongeza ufanisi wa kufanya biashara. 

“Programu hii inatarajiwa kupunguza usumbufu, kuongeza uwajibikaji na uaminifu kwenye sekta na mifumo ya biashara. Pia, itasaidia kupanua wigo wa soko la dunia kwa kuruhusu na kurahisisha biashara kufanyika mkononi kutoka mahali popote ulipo,” alisema. 
Waziri Mkuu pia alizindua mfumo wa JIBA Sandbox ambao unalenga kuwawezesha wadau kupata mafunzo na elimu ya jinsi kufanya biashara kwa ufasaha na kujikuza kwenye biashara na soko ulimwenguni. Pia alizindua maktaba mtandao (JIBA Investment Desk) ambayo itashughulika na utoaji wa taarifa za mifano ya biashara kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ufugaji wa samaki, kilimo kwa kutumia mfumo wa kisasa wa akili bandia (artificial intelligence). 

Ili kuhakikisha programu hizo zinakuwa endelevu na zinatoa matunda yaliyokusudiwa, Waziri Mkuu aliitaka timu ya uongozi wa JIBA na wanachama wake waiunge mkono Serikali katika kuongeza wigo wa utoaji elimu ya fedha kwa vijana na kuwawezesha kutumia vizuri mitaji wanayoipata kwa ajili ya biashara. 

“Vilevile, wawezesheni kutumia vema fursa mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza kwenye maeneo yao. Tengenezeni nafasi kwa vijana kupata fursa ya mafunzo ya uzoefu wa kazi kwenye kwenye taasisi na biashara zenu na hivyo kuwasaidia kujiajiri au kuwapatia ajira,” alisema.

 Aliwataka washirikiane na Serikali kuibua vipaji kwenye eneo la sayansi na teknolojia, kuwaendeleza na kuwatumia wabunifu wa Kitanzania kama wanavyofanya kwa JIBA App. “Tungejisikia fahari kuona programu kama hizi ambazo tumezindua leo zinabuniwa na kujengwa na vijana wetu,” alisema.

Akielezea hatua zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), imefanya maboresho makubwa ikiwemo kupunguza baadhi ya vigezo ambavyo vilikuwa ni kikwazo kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza nchini hususan kupata Cheti cha Vivutio vya Biashara (Certificate of Incentives). 

“Kabla ya maboresho hayo, iliwalazimu Watanzania wawe na miradi yenye thamani isiyopungua dola za Marekani 100,000, yaani shilingi milioni 235 ili wafuzu kupata Cheti cha Vivutio. Hata hivyo, kuanzia mwaka jana, Serikali imefanya mapitio na kiwango hicho kimepunguzwa kwa asilimia 50. Hivi sasa, mradi wa dola za Marekani 50,000 sawa na shilingi milioni 117,500 unafuzu kupata Cheti cha Vivutio cha TIC.” 
Alisema Serikali itaendelea kufanya maboresho ya kitaasisi, kisera na kisheria kwa lengo la kuimarisha shughuli za uwekezaji na biashara nchini. “Tumieni fursa hiyo kuibua changamoto za kisheria, kikodi na nyinginezo na kuwasilisha kwa Serikali kwa ajili ya hatua za maboresho na utatuzi,” alisisitiza. 

Mapema, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar bin Zubeir Mbwana alisema suala la biashara kuwa uti wa mgongo wa maisha ya mwanadamu linasisitizwa sana kwenye Quran tukufu. “Sehemu tisa katika mafungu 10 ya riziki yako katika biashara na ukulima na moja ya kumi iliyobaki iko katika ufugaji. Sura nyingine inasema Mwenyezi Mungu anapenda kumuona mja wake anasumbuka kutafuta riziki ya halali.” 

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara wakubwa wajihadhari na suala la ushoga ambalo hivi sasa limeenea duniani ili kuepuka ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. “Ninyi ni wafanyabiashara wakubwa, mliangalie suala hili sababu Mwenyezi Mungu anachukizwa, mkiacha liendelee tunaweza kupata balaa huko mbeleni. Kama zamani waliangamizwa kwa kosa hilohilo, haiwezekani na sisi tusiangamizwe na Mwenyezi Mungu kama tutaliruhusu,” alisisitiza. 

Naye, Mwenyekiti wa JIBA Tanzania, Bw. Al Junaid Hasham alisema taasisi hiyo iliyosajiliwa Uingereza ina matawi 32 duniani kote na lengo lake kuu ni kukuza fursa za kibiashara kwa wanajamii wa Khoja na wanachama washiriki (associate members). 

Alisema wanatarajia kuanzisha jukwaa la kibiashara kupitia programu za JIBA App na JIBA Investment Desk na kwamba wanataka kuifanya Tanzania iwe kitovu cha wafanyabiashara ulimwenguni kote. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news