Tanzania,Jumuiya ya Madola kushirikiana kukabili changamoto za kidunia

NA MWANDISHI WETU

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeahidi kushirikiana na Jumuiya ya Madola kukabiliana na changamoto za kidunia zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, Uviko 19, migogoro, ugaidi na umasikini.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo azungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. David Concar pamoja na Balozi wa Rwanda nchini, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba alipowasili katika makazi ya Balozi wa Uingereza jijini Dar es Salaam.

Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo aliposhiriki maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo akiwasilisha hotuba yake katika maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Balozi Shelukindo amesema licha ya uhusiano wetu na historia ya pamoja kama wanachama wa Jumuiya ya Madola tunaamini kuwa kwa umoja wetu tunaweza kuzikabili changamoto za kidunia kwa urahisi zaidi.

“Kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake kwa wakati, itakuwa rahisi kuzikabili changamoto za kidunia hususan mabadiliko ya tabianchi, Uviko 19, migogoro, ugaidi na umasikini,” alisema Balozi Shelukindo.
Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. David Concar akiwasilisha salamu za Jumuiya ya Madola wakati wa maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza hapa Nchini, Mhe. David Concar amesema Jumuiya ya Madola imekuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania hususan vijana ambao ndiyo taifa la kesho wamekuwa wakinufaika na ufadhili wa masomo kwa ngazi mbalimbali, biashara na uwekezaji pamoja na ajira.

Balozi Concar amesema Jumuiya ya Madola imefurahishwa na hatua ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikizichukua katika masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ulinzi na usalama na utawala wa sheria. 

“Tanzania imeboresha sana masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ulinzi na usalama na utawala wa sheria….. mtakumbuka hivi karibuni mikutano ya kisiasa imeruhusiwa pamoja na uhuru wa vyombo vya Habari umeongezwa jambo ambalo linaashiria kukua na kukomaa kwa demokrasia,” alisema Balozi Concar.
Balozi wa Uingereza hapa Nchini, Mhe. David Concar akichangia jambo wakati wa maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Balozi Concar ameongeza kuwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya biashara na uwekezaji nchini na hivyo kuchangia uchumi wa Tanzania kukua. 

Maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yamehudhuriwa pia na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba pamoja na baadhi ya wanamichezo wa Tanzania walioshiriki kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Picha ya pamoja.
Maadhimisho yameongozwa na Kauli Mbiu isemayo ‘Kujenga mustakabali endelevu na wenye amani wa pamoja’.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news