BENKI YA DUNIA:Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika

NA LWAGA MWAMBANDE

MRUGENZI Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruko ameipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayopata fedha kutoka kwenye taasisi hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Dkt.Ngaruko ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaoongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) jijini Washington, Marekani.

Aidha, Dkt.Ngaruko, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya Dunia katika ukanda huo, alisema kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, tathimini ya benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.

“Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano kwa usimamizi mahiri wa masuala ya uchumi mpana, si tu kwa nchi za Afrika Mashariki, bali kwa nchi za Afrika, ambapo kiwango cha ukuaji uchumi cha wastani wa asilimia 5.4 ni cha juu, na ninawapongeza sana,”alisema Dkt.Ngaruko.

Pia, alipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa benki yake itaendelea kuisaidia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi. 
 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anafafanua kuwa, ni ishara njema kuona Benki ya Dunia inasifia juhudi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mikakati thabiti ya kustawisha uchumi wake. Endelea;

1.Hiyo Benki ya Dunia, ndiyo inatusifia,
Habari tumesikia, moyo kweli zatutia,
Kumbe tukichakatia, huko kwao twanunikia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

2.Uchumi kusimamia, pesa vema kutumia,
Hao walinganishia, na kwingineko pia,
Inang’ara Tanzania, yake Rais Samia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

3.Sera kwa kusimamia, uchumi za fedha pia,
Sifa kubwa Tanzania, huko imejipatia,
Yafanya mambo kwa nia, pema tuweze fikia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

4.Hiyo Benki ya Dunia, data zote hupitia,
Na pia huangalia, na maendeleo pia,
Dole imeipatia, nchi yetu Tanzania,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

5.Sana wameangalia, nchi yetu Tanzania,
Jinsi ilivyopitia, UVIKO lipoingia,
Buti ilijikazia, bila hata kutitia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

6.Changamoto vita pia, Ukraine na Russia,
Tanzania yabakia, kiuchumi yatumia,
Uchumi wainukia, kwa hali ya kuvutia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

7.Huku si kujisifia, wengine watusifia,
Wale wanaangalia, bila ya nia kutia,
Mema wanatutakia, pema tuweze fikia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

8.Uchumi mpana pia, kongole kwa Tanzania,
Huko ndivyo wasifia, kule Benki ya Dunia,
Viashirio sikia, vyote wanaangalia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

9.Waziri wa Fedha pia, na Mipango Tanzania,
Hongera kazisikia, na yeye zimemwingia,
Tena kawasimulia, vema tunajifanyia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

10.Mwigulu kamsifia, Rais wetu Samia,
Jinsi anasimamia, nchi yetu Tanzania,
Hatua twajipigia, kuzuri tutafikia,
Kongole kwa Serikali, kazi inatambulika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news