MAKUNDI YA DAMU, KANZIDATA NI MUHIMU

NA LWAGA MWAMBANDE

APRILI 11, 2023 Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema Serikali inadhamiria kuanzisha Kanzi Data ya kutambua makundi ya Damu kwa Watanzania wote.

Lengo la Serikali kufanya hivyo ni ili kusaidia kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa damu salama kwa watu wenye makundi adimu ya damu.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mpango wa Taifa wa Damu Salama jijini Dar es Salaam, kwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, wanayo kanzi Data ya Watu takribani 350 ambao wapo kwenye Kundi O-Negative baada ya kuwatambua kama kundi adimu la damu.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,kanzi data kupitia makundi ya damu nchini ni jambo jema ambalo linapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote. Endelea;

1. Hii nayo kanzidata, kwa kweli ni ya muhimu,
Shida hii tunapata, ifike iwe adimu,
Mahitaji tukipata, huduma ziwe muhimu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

2. Ametangaza Waziri, wa Afya jambo muhimu,
Tena yeye amekiri, hili huleta ugumu,
Kukiwepo na hatari, makundi damu adimu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

3. Yako makundi ya damu, wenyewe wako adimu,
Kama kiishiwa damu, kupata huduma ngumu,
Lakini tukifahamu, tutapunguza ugumu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

4. Magonjwa tukiyapata, ikahitajika damu,
Kule tunakoipata, wala siyo kila damu,
Ni vipimo vinapita, kundi sawa kufahamu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

5. Endapo kundi adimu, kupatikana wagumu,
Hapo sote twafahamu, hatari hiyo yadumu,
Tukikosa mwanadamu, maisha hawezi dumu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

6. Tuzidi kutoa damu, hiyo kitu ni muhimu,
Magonjwa tunafahamu, muda wowote yatimu,
Ikihitajika damu, kukosa kifo chatimu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

7. Mnaochangia damu, maisha mzidi dumu,
Mwaokoa wanadamu, ambao wasingedumu,
Jambo kubwa twafahamu, hata kwake Mungu tamu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

8. Bure tunapewa damu, Mungu ndiye afahamu,
Kutoa bure tudumu, tuokoe wanadamu,
Watibike na wadumu, kufanya mambo muhimu,
Haya makundi ya damu, kanzidata ni muhimu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news