DCEA, TAKUKURU zakubaliana kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), zimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya na kupiga vita vitendo vya rushwa nchini.
Taasisi hizo zimefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa hutumia rushwa kufanikisha usafirishaji wa dawa za kulevya ambapo wamekuwa wakiwahonga watu wasiowaaminifu ili wawasaidie kukamilisha uhalifu huo katika maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi.

Ushirikiano huo utajikita zaidi katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya na kupiga vita rushwa kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuoni kupitia klabu za kupiga vita rushwa mbazo sasa zitatumika kupiga vita rushwa na dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema kuwa,mamlaka katika kuendeleza mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya nchini, imeona ni vema ikashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kupanua wigo wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya. 

Ameeleza kuwa,ushirikiano huo ni muhimu kwani utaisaidia sehemu kubwa ya jamii hasa wanafunzi ambao baadhi yao kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya wakiwa katika umri mdogo, kufahamu madhara ya dawa za kulevya na hatimaye kutoshiriki kwenye matumizi na biasha ya dawa hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, CP.Salum Rashid Hamduni, ameeleza kuwa, anatambua ushirikiano baina ya taasisi hizo utaleta tija katika mapambano dhidi ya rushwa na tatizo la dawa za kulevya nchini. 
 
Amehimiza kuwa, ni muhimu taasisi hizo zikajipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa jukumu hilo linatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. 
Aidha, amesema kuwa, ushirikino huo usijikite tu katika utoaji wa elimu juu ya Rushwa na Dawa za kulevya bali pia katika kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana makosa ya rushwa, kwani ni wazi kuwa, idadi kubwa ya watu wanaokutwa na makosa hayo pia hukutwa na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Makubaliano hayo yamefanyika leo Aprili 14, 2023 jijini Dodoma, katika Ofisi za Makao Makuu ya TAKUKURU yaliyohudhuriwa pia na baadhi ya Maafisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news