Majizzo afunguka huku akiwatakia kila la heri Maulid Kitenge, Gerald Hando, B Dozen na Oscar Oscar

NA DIRAMAKINI

AFISA Mtendaji Mkuu wa E-FM Company Limited ambayo ni kampuni binafsi inayomiliki kituo cha runinga cha TVE na kituo cha Redio cha E-FM,Francis Antony Ciza (Majizzo) amewatakia kila la heri waliokuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo,Maulid Kitenge, Gerald Hando, B Dozen na Oscar Oscar.

Tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo mwaka 2014 ikiwa na makao yake makuu jijini Dar es Salaam, ndani ya miaka tisa imetajwa mara nyingi kuleta mageuzi makubwa katika tasnia ya habari hususani kupitia matangazo ya redio na runinga.

"Ilikuwa wakati mzuri sana kufanya kazi na ndugu zangu Maulid Kitenge, Gerald Hando, B Dozen na Oscar Oscar. Nitaendelea kuwashukuru na kuwaheshimu sana kwa mchango walioweka hapa EFM na TVE.

"Nawatakia mafanikio katika ajira zao mpya, mafanikio yao ni mafanikio ya tasnia na hiyo ni furaha yangu.All the best ndugu zangu.MuzikiUnaongea,"amefafanua Majizzo kupitia ukurasa wake wa Instargram.

Ikumbukwe kuwa,Desemba 11, 2015 kwa mara ya kwanza nchini Tanzania ilikuwa ni siku ambayo haiwezi kusahaulika kwa radio changa na bora kama EFM ambayo inatangaza kutoka jijini Dar es Salaam kutwaa tuzo ya mwaka kwa ubunifu na ubora wa vipindi.

Tuzo hiyo ilitolewa katika Hoteli ya Hyatt Regency ambako waandaaji wa tuzo hiyo, Tanzania Leadership Awards chini ya usimamizi wa taasisi maarufu ya Kimataifa-Purple Cow waliweza kuiandika historia ya EFM nchini Tanzania.

Waandaaji wa tuzo hiyo, walitumia vigezo sahihi vya utoaji tuzo kwa kila mtu au kampuni ambazo zilifanya vizuri katika biashara kwa mwaka 2015

Aidha, katika kampuni zote za biashara zilizoingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho, EFM iliibuka kidedea ikiwa na miezi 18 tu tangu kuanzishwa kwake na ilionesha mafanikio makubwa kutokana na jitihada zake katika utendaji kazi hali ambayo haikushangaza wengi na hivyo ikafanya kuwa ya kwanza ikifuatiwa na TBC Taifa.

Baada ya kamati kuu kukaa na kutathmini, pamoja na kura zilizopigwa na watu walioshiriki, 93.7 EFM radio ilichaguliwa kuwa kituo bora cha redio cha mwaka. Jitihada za kufanya ubunifu na maboresho zaidi ziliendelea hadi kuzaliwa runinga ya TVE.

Wakati huo huo, Majizzo ameendelea kufafanua kuwa, "Telescope ni kifaa cha kipekee kilichosaidia uvumbuzi wa mengi, kifaa chenye matumizi ya thamani kubwa lakini kimetengezwa katika saizi tofauti kiweze kumilikiwa na wengi.

"Maisha yangu yemekuwa hivyo, nimekuwa nikimuomba Mungu niweze kuona mbali kama Telscope, lakini nisiwe mwenye kujikweza ili Watanzania wenzangu wa kawaida kabisa, wale wa kule uswahilini na kwingine kugumu nilikotoka wajue mimi ni mwenzao. Asante Mungu, imeendelea kuwa hivyo.

"Miaka 9 iliyopita tuliona thamani kwa Watangazaji, thamani ambayo kwa wengine ilipuuzwa sana. Tukakuza majina yao na kuyalinda, na sasa nina furaha sana kwamba thamani niliyotamani waipate wanaipata.

"Muda umefika, redio zinahitaji ladha mpya, tunahitaji kutoa nafasi kwa vijana wapya, hatuwezi kuwa na sauti zilezile kila mahali. Kama ambavyo nimeongea mara nyingi, mimi nitatoa nafasi kwa vijana wapya.

"Lakini mtakubaliana nami kuwa hii ni biashara na inahusisha mchakato kama vitu vingine, lazima tuanzie mahali twende kwa hatua nzuri.

"Tuanze na watu ambao tunawajua, lakini hatujui upande wa pili wa vipaji vyao. Masanja tunamjua kama mchekeshaji na kwenye ‘media’ yuko upande wa mahubiri tu. Hatujamuona akisoma magazeti.

"Kama ambavyo tulitambulisha mtindo mpya wa kusoma magazeti ambao hivi sasa unaigwa sehemu nyingi, leo tunatambulisha msomaji mpya wa magazeti katika namna ya kuvutia. Namleta kwenu Masanja Mkandamizaji, #KunyamvuaKunyumbulishaNaKukandamiza.Karibu #JotoLaAsubuhiEFM,"amefafanua Majizzo katika kumtambulisha mtangazaji Masanja Mkandamizaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news