Musoma wafunguka kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia

NA DIRAMAKINI

WANAWAKE wa Kijiji cha Kome Kata ya Bwasi katika Halamashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara wameiomba Serikali kuanzisha dawati la ulinzi na usalama dhidi ya wanawake na watoto. 
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na wanawake hao wakati wakifanya mjadala dhidi ya hali ya vitendo vya ukatili wa kijinsia uliozoeleka katika kijiji chao na namna jamii inavyoweza kutatua changamoto hizo ndani ya eneo husika.

Akiongea katika mjadala huo, Christina Masamaki alipendekeza kuanzishwa kwa dawati hilo ili kuweza kuratibu na kuchukua hatua dhidi ya wale wanaotenda ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike ikiwemo mimba za utotoni.

Alisema, wahanga wa vitendo hivyo hukosa haki kutokana na wazazi kulipana kwa makubaliano wakati wahanga wakibaki katika mazingira duni ikiwa ni pamoja na kushindwa kuendelea na masomo yao.

"Wapo wasichana zaidi ya wawili katika kijiji hiki ambao wamepata mimba nawafahamu wakiwa shuleni na wazazi wao wamelipwa na walio tenda ukatili huo wapo, sisi kama wanajamii hatuna uwezo wa kuingilia jambo hilo japo Wasichana hao wamebaki hapa kijijini wakitaabika,"amesema mmoja wa wanawake hao.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kome, Benedictor Daudi alisema atashirikiana na akinamama hao ili dawati hilo liweze kuanzishwa kutokana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kukithiri kijijini hapo, ambapo pia alisema mara nyingi wazazi hulipana kwa njia ya makubaliano bila wahusika kufikishwa katika vyombo vya kisheria. 
Mjadala huo ulioandaliwa na Shirika la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) kupitia mradi wake wa 'Funguka paza Sauti kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia uliozoeleka katika maeneo ya Uvuvi' unaotekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil society. 

Ajirathi Hisein alisema, wanawake hasa wasichana wamekuwa wakidharirishwa kwa kupigwa na kuchaniwa mavazi hadhani hasa nyakati za sherehe za kijamii na vijana kwa madai kuwa wamewapatia fedha kwa ajili ya kufanya nao mapenzi na kisha huwakatalia.
"Pamoja na kuwa udharirishaji huo unafanyika hadharani hakuna msaada unaopatikana kutoka kwa wanajamii, lakini tukiwa na dawati litakuwa na nguvu za kisheria kuchukua dhidi ya wanaotenda unyama huu,"alisema Ajirathi huku akiungwa mkono washiriki.

Ukatili mwingine uliobainishwa kuwa umekithiri ni utelekezaji wa familia ambao umeelezwa kufanywa na jinsi zote wanaume na wanawake kwa kukimbia ndoa zao na kwenda Vizingani kwa shughuli za Uvuvi na biashara mbalimbali huku wakiwaacha watoto kijijini hapo wakitaabika.

Mimba za utoto, utoro na kuacha shule ni baadhi ya aina za Ukatili uliozoeleka ambao ulitajwa na wakazi hao wa kijiji cha Kome .
Kwa upande wake Mratibu wa Miradi huo Robinson Wangaso alisema mjadala huo pia umefanyika katika Kijiji cha Busekera kata ya Bukumi ambapo Ukatili wa kiuchuni kwa akinamama wanaofanya shughuli za kuchakata Samaki wametaja kudhurumiwa na wale wanaowajiri ambao ni wachuuzi wa samaki.

Wangaso alisema uongozi wa Kijiji cha Busekera kupitia mwenyekiti wake Paineto Bwire na Mwenyekiti wa Umoja wa wasimamizi wa Mwalo BMU ndugu Daddy Rashird Ndege ambao pia walishiriki katika mjadala huo waliahidi kushirikiana na akina mama wanao chakata Samaki kuanzisha umoja wao ili kuweza kudai hali zao kwa pamoja tofauti na sasa.

"Tunaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa kijamii, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kushughulikia vitendo vya ukatili Ukatili wa kijinsia uliozoeleka katika jamii za Wavuvi licha ya kuwa juhudi na nguvu za wadau wengine zinahitajika kwani mradi wetu unazo rasilimali kidogo ukilinganisha na halisi ilivyo mahitaji ni makubwa sana,"amesema Wangaso.

Washiriki wa mjadala huo walilishukuru shirika la VIFAFIO kwa namna ambavyo limeweza kuwafikia kuwapa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia uliozoeleka maeneo ya mialo kwani itawasaidia kuhakikisha vitendo hivyo havipati nafasi kwani ni kinyume Cha Sheria na haki za binadamu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news