Mwinjilisti Alphonce Temba ampa kongole Rais Dkt.Samia kwa kufanikisha Bandari kavu Kwala

NA GODFREY NNKO

MWINJILISTI wa Kimataifa, Alphonce Temba ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani.
Temba ametoa pongezi hizo baada ya kufika ilipo bandari hiyo na kushuhudia mafanikio makubwa ambayo amesema, uwekezaji huo ni hatua njema na ustawi bora kwa Taifa na jamii kwa ujumla.

"Nimefika katika Bandari ya Kwala ambayo itahudumia mataifa mbalimbali. Serikali imefanya kazi kubwa, chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ndiyo maana unaona sasa hivi uchumi unaenda kukuwa. 

"Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Uchukuzi ametuambia kwamba,zaidi ya makontena 75,000 hadi 100,000 yatapatikana kwa mwaka, mizigo inaingia bandarini, itakuja mahali hapa.Mama umefanya kazi kubwa, tunakupongeza sana, Watanzania ni wakati wa kuhamka sasa, fursa zipo Kwala.

"Vigwaza, Chalinze, Kibaha na Pwani kwa ujumla. Zaidi ya ajira milioni moja za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinaweza kupatikana, tunakupongeza mama kwa kazi kubwa unayoifanya. Kwa kweli nimeshuhudia mambo makubwa sana ambayo yanafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
 
"Mama anafanya kazi kubwa, kwa ustawi bora wa Taifa letu, jamii na wanananchi kwa ujumla, hivyo tutaendelea kumuunga mkono ili kuhakikisha maono yake ya kuliwezesha Taifa kuwa na maendeleo endelevu na kutekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatimia kwa wakati,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Amesema, Rais Dkt.Samia amekuwa akipambambania na kutoa fedha nyingi kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezeka kwa wakati ili iweze kutoa huduma kwa wananchi na kuhudumia mataifa ya nje.

"Bandari ya Kwala imetumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwatengenezea Watanzania fursa na kuweza kuhudumia mataifa zaidi ya saba Afrika yanayoizunguka Tanzania. Hivyo, ninakupongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa hatua hii njema,"amefafanua Mwinjilisti Temba. 

Uchukuzi

Hivi karibuni Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuz, Dkt.Ally Possi amezitaka taasisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli (TRC) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili kuanza kutumia Bandari kavu ya Kwala kwani kwasasa ujenzi wa Bandari hiyo umefikia asilimia 98. 

Possi aliyasema hayo kwenye kikao kilichowakutanisha wafanyabishara wa Bandari, Wizara , TRC na TRA, katika kuboresha utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam. 
“Ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala umefikia asilimia 98, hivyo taasisi zote zinatakiwa ziwezeshwe kuhamia ili kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam,”amesema Dkt.Possi. 

Aidha, Dkt. Possi amezielekeza taasisi hizo kutoongeza gharama katika kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Saalam mpaka Kwala, kwani kuongezeka kwa gharama kutaongeza wafanyabiashara kutotumia bandari hiyo. 

Baadhi ya wafanyabiashara katika sekta ya bandari wamesema kuwa wapo tayari kutumia Bandari ya Kwala kwani bandari hiyo itasaidia kupunguza mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, hivyo wanaomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), kuendelea kusimaia mifumo ya utoaji huduma ili kusiwe na usumbufu. 
Naye Meneja Uendeshaji kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Focus Sahani amesema tayari shirika hilo limeshatenga mabehewa pamoja na vichwa vya treni kwa ajili ya kuanza kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kwala. 

Kwa upande wake Meneja Msimamizi wa Ujenzi wa bandari hiyo, Alexander Ndibalema amesema kuwa, ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara ya kilometa 15 kutoka Vigwaza mpaka Kwala umekamika, hivyo bandari hiyo ipo tayari kuanza kazi. 

Waziri Mkuu

Aprili 5, 2023 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 aliigusia Bandari Kavu ya Kwala.
"Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Mradi wa Bandari Kavu ya Kwala ambapo ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa kilomita 15.5 kutoka Vigwaza umefikia asilimia 98.

"Kukamilika kwa bandari hiyo na kuanza kutumika kutapunguza msongamano wa mizigo na magari katika bandari ya Dar es Salaam, kuongezea nafasi ya kuhifadhi mizigo na kupunguza muda wa magari kusafirisha mizigo. 

"Hali hiyo itaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na hivyo kuongeza mapato kwa bandari na wafanyabiashara.

"Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, sekta ya usafiri na usafirishaji itaendelea kukamilisha ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma za usafiri kwa njia reli, anga, barabara na majini. 

"Aidha, Serikali imeamua kwa dhati kuanza ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kwa kuhamisha wananchi waliolipwa fidia, wanaotakiwa kupisha ujenzi wa bandari na kuanza maandalizi ya ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya bandari ya Bagamoyo ikiwemo barabara, reli na umeme,"alifafanua Mheshimiwa Waziri Mkuu. 

Burundi

Aidha, miongoni mwa mataifa yatakayonufaika na huduma za Bandari Kavu ya Kwala ni Burundi ambapo Oktoba, mwaka juzi Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye alitembelea bandari hiyo mkoani Pwani.
Mhe.Ndayishimiye alisema kuwa, eneo la bandari kavu (Kwala) litakuza biashara kati ya Tanzania na Burundi na litawasaidia kupunguza gharama za usafiri na fedha zitakazookolewa zitaenda kwenye miradi mingine.

“Mradi huu pia utapunguza gharama za bidhaa mbalimbali nchini Burundi, kwetu sisi Burundi, mtu akikupa eneo amekuthamini sawa na kukuunga undugu kwenye familia yake,”alisema Mhe.Ndayishimie.

Awali akitoa taarifa ya eneo hilo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (Mb) alisema eneo hilo lina ukubwa wa hekta 502, kati ya hizo hekta 10 zimetengwa kwa ajili ya Serikali ya Burundi.

“Dhumuni la kutenga eneo hili ni kupunguza msongamano wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam,”alisema Prof. Mbarawa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news