Serikali yatoa maagizo kwa maafisa elimu nchini

NA FRED KIBANO

MAAFISA Elimu wa mikoa na halmashauri nchini wametakiwa kuwasimamia walimu kwa weledi na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuleta mabadiliko katika Sekta ya Elimu nchini.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa hivi karibuni jijini Mwanza na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU), Dkt. Charles Msonde wakati akitoa maelekezo ya Serikali kwa Viongozi hao kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri (REDEOA).

Dkt. Msonde amesema njia pekee ya kuleta mabadiliko kwenye Sekta ya Elimu ni uwajibikaji wa kuwasaidia walimu kukabiliana na changamoto zinazowakabili kwenye mazingira yao ya kazi kama vile kuwa na kanuni ya ulipaji wa madeni ya walimu na kuyakabili masuala yote yanayohusiana na rushwa sehemu ya kazini.

“itakuwa ni kazi ngumu sana kwa walimu kuhubiri mabadiliko kama walimu hawa hatujawajali, changamoto za walimu ni nyingi na mazingira yao ya utendaji kazi yanahitaji sisi tuwasaidie zaidi,” amesema Dkt. Msonde.

Amesema kuwasimamia walimu katika ufundishaji unaozingatia watoto kupata ujuzi ambao utaleta matokeo makubwa kuliko ufundishaji wa kuzingatia kumaliza mada kwa wakati bila kuzingatia malengo ya Mkakati wa Ufundishaji na vigezo vyake 22 kama Kusoma, Kuandika na kuhesabu na umahiri katika somo la kiingereza kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Dkt. Msonde amewapongeza Viongozi hao kwa kuongeza kiwango cha uwajibikaji wa walimu nchini kutoka asilimia 30 iliyokuwepo hapo awali mpaka asilimia 60 iliyopo hivi sasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Vicent Kayombo amesema kwa hivi sasa Viongozi hao wanafuatilia kwa karibu ufundishaji wa walimu shuleni lakini pia ili kuboresha Ufuatiliaji na Usimamizi wa elimu tayari magari yaliyoagizwa kwa ajili ya Seksheni ya Elimu ya Sekondari yameshawasili na yatapelekwa kwenye maeneo husika.

Kauli Mbiu ya Mkutano huo kwa mwaka 2023 wa REDEOA unasema ‘Uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu Unaimarisha Ufundishaji, Ujifunzaji na Ustawi wa Walimu na Wanafunzi’.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news