Rais Dkt.Mwinyi aendelea kusisitiza maadili mema nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuiasa jamii kuendelea kuwajengea uwezo vijana ili kukuza jamii yenye maadili mema na hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu (S.W.)
Rai hiyo ameitoa leo Aprili 19, 2023 katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar kwenye hafla ya mashindano ya Quran tukufu kwa njia ya Tartil.
Mheshimiwa Rais amesema, kumekuwa na mporomoko wa maadili na kupotea kwa sehemu kubwa ya mila na silka za Wazanzibari, hivyo ameeleza kupitia utaratibu wa kuwahifadhisha vijana Quran tukufu ni njia ya kuzalisha viongozi bora wa baadae wakiwemo Masheikh na Maulamaa.

Amesema, hatua hiyo pia inahamasisha jamii juu ya kuendelea kukisoma kitabu kitukufu cha Quran ambacho ndani yake kuna faida nyingi zikiwemo kukisoma, kukisomesha na kukihifadhi.
Katika hafla hiyo, pia Alhaj Dkt.Mwinyi ametoa zawadi ya shilingi milioni moja kwa kila mshindi, kwa washindi watano wa mwisho ikiwa ni zawadi za ushiriki wao kwenye mashindano hayo, pia ameitaka jamii iendelee kuhamasisha vijana wengi kwenye mashindano yajayo ili kukisoma vyema kitabu kitakatifu cha Quran.
Alhaj Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuziomba sekta binafsi kuungana na sekta za umma kutoa mapema mshahara wa mwezi Aprili, mwaka huu baina ya leo Aprili 19 na kesho Aprili 20 ili kuwapa muda wa kutosha wafanyakazi wao kwa maandalizi ya sikukuu ya Eid Fitri inayotarajiwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, maombi hayo yamekuja kufuatia maagizo aliyoyatoa Apirili 16, mwaka huu kwa taasisi zote za umma kuwapa mapema mshahara wa mwezi huu watumishi wa umma ili wafurahie vizuri sherehe za sikukuu, baada ya Mfungo mtukufu wa Ramadhan.

Amesema, baada ya maagizo yake alipokea maombi mengi kutoka kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ili nao wafaidike, lakini kwa vile hana mamlaka na sekta binafsi, aliziomba sekta hizo waridhie maombi yake na wawape mishahara wafanyakazi wao baina ya leo na kesho.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesifu juhudi za Rais Alhaj Dkt.Mwinyi katika kuunga mkono na kuendeleza masula ya khairati nchini.
Pia amesema tokea kunza kwa Mfungo mtukufu wa Ramadhan, Alhaj Dkt.Mwinyi amefanikiwa kufutarisha nchi nzima kwa mikoa yote ya Unguja na Pemba, aidha, aleleza taifa limemshuhudia akishiriki ibada za sala za pamoja na wananchi wake zikiwemo Ijumaa na Taraweikh kwa kipindi chote cha swaum kwa maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa huduma za kibenki kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Said Muhamed Said amesema, benki hiyo haiko nyuma kwenye kujikita na masuala ya jamii ili kuendelea kuwa karibu na wateja wake. 

Amesema, PBZ ina wajibu wa kushirikiana na Serikali kwenye kupata vijana wenye maadili mema pamoja na kuiunga mkono serikali kukuza na kuendeleza maadili ya vijana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi ufungo wa gari aina ya Toyota Alphard mshindi wa kwanza wa Fainali ya Mashindano ya Kusoma Qur-an Tartiil Zanzibar, mwanafunzi Said Ali Juma, baada ya kuibuka mshindi katika mashindano hayo ya fainali yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja jijini Zanzibar leo. Na kulia kwa Rais ni Mkurugenzi Huduma za Kibenki PBZ, Said Mohammed Said.

PBZ ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo waliiomba jamii kuendelea kuitumia ili na wao waendelee kuunga mkono shughuli za jamii.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazi Zanzibar (ZBC), Salum Ramadhan Abdalla Shaaban ambao ni waratibu wa mashindano hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo amesema, mashindano hayo yalianza mwaka jana baada ya kuzaliwa wazo na ZBC kabla ya kuliwasilisha Wizara ya Habari ambayo mafanikio yake yamekuwa endelevu hadi sasa.
Washiriki wa Fainali ya Mashindano ya Kusoma Qur-an Tartiil, wakiwa katika ukumbi kabla ya kuaza kwa mashindano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja jijini Zanzibar, yaliyodhaminiwa na Benki ya Watu wa Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar yaliibua washindi watatu, mshindi wa kwanza alizawadiwa gari aina ya Alphad, mshindi wa pili bodaboda na mshindi wa tatu fedha taslimu shilingi milioni mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news