Rais Dkt.Mwinyi asisitiza malezi na maadili mema kwa watoto wote

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amehimiza jamii kujikita kwenye malezi yenye maadili ya kiislamu kwa watoto na vijana ili wawe na tabia njema zitakazomridhisha Mwenyezi Mungu (S.W).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsalimia Mzee wa Kijiji cha Dunga baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Al-Jumaa Dunga Kiembeni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja leo.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt.Mwinyi ametoa nasaha hizo wakati wa ufunguzi wa msikiti wa masjid Al - Jumaa, uliopo Dunga Kiembeni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema, jamii imeghubikwa na wingu la matatizo yanayosababishwa na mporomoko wa maadili, kujaa madhila ya udhalilishaji, kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya, wizi wa mazao ya kilimo na mifugo kulikosababishwa na kukosa malezi bora yenye hofu ya ucha Mungu na ukosefu wa maadili.
“Vijana wetu wafundishwe dini yao vizuri, wafundishwe kitabu cha Mwenyezi Mungu, wafundishwe tabia njema, tutapunguza matatizo yanayotokea ukubwani,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Alhaj Dkt.Mwinyi pia amezisihi jamii kutumia nyumba za ibada kuwafundisha vijana mustakbali mwema wa ustawi wa maisha yao kupitia madrsa na nyumba za ibada ikiwemo misikiti, aliongeza malezi hayo yanaanzia kwenye nyumba za ibada ili kuondosha matatizo yanayoisumbua jamii.

Akieleza neema za mwezi mtukufu wa Ramadhani, Alhaj Dkt.Hussein Mwinyi amewasihi wanajamii kuzingatia ibada na kujitahidi kwenye kuongeza ibada ya sala za taraweikh aliyoieleza kwamba inakuja mara moja tu kwa mwaka pamoja na kuwasihi waumini wa msikiti huo, kuendeleza ibada za sala za sunnah. 

Hata hivyo, Alhaj Mwinyi ameahidi kuujengea uzio msikiti huo ili uiendaene na hadhi yake na uendelee kudumu na kuwa imara.

Wakati huo huo,Alhaj Dkt.Mwinyi amewataka waumini wa msikiti huo kuendelea kuutunza na kuuenzi ili udumu kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadae.

Akizungumza kwenye ibada hiyo ya sala ya Ijumaa, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume amewasihi waumini wa dini ya kiislamu kuutumia vyema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kujitathmini na kujipima mema na mabaya yao mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuongeza bidii ya kufanya ibada hasa kwa siku chache zilizobakia kabla ya kumalizika kwa ibada ya mfungo wa mwezi huo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la ufunguzi wa Masjid Al-Jumaa Dunga Kiembeni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, ufunguzi huo umefanyika leo Aprili 7,2023.(Picha na Ikulu).

“Huu ndio mwezi wa kheri na kufanya mazuri zaidi yatakayompendezesha Mwenyezi Mungu, ili kupata msahama wake na sio kupoteza muda na kuanzisha michezo isiyo na tija kwenye jamii,"ameshauri Katibu huyo.

Mapema akisoma risala ya ufunguzi wa msikiti huo, Ustadhi Abdalla Makame Makame amesema ujenzi wa msikiti ulichukua miezi minne tokea kunza hadi kukamilika kwake.

Alieleza ulianza kujengwa Novemba 11 mwaka 2022 na ulikamilika Machi 13, 2023 ambapo unatarajiwa kuchukua hadi waumini 612. 

Pia alieleza ujenzi wa msikiti huo ulikuja kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ikiwemo ufinyu wa nafasi kwa msikiti wa awali uliosababishwa na kuongezeka kwa waumini wengi kijijini hapo, baadhi yao wakiwa wahamiaji katika eneo hilo.

Ustadhi Makame aliongeza sababu nyingine ya kujengwa kwa msikiti huo ni kupisha utanuzi wa ujenzi wa barabara inayotarajiwa kutoka Dunga Mitini kuelekea Chwaka.

Hata hivyo, ujenzi wa msikiti wa masjid Al-Jumaa uligharimu shilingi milioni 178.148 ambao ulifadhiliwa na shekh Said Saleh.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news