Rais Dkt.Samia aridhia msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi Bilioni 21.3/- kwa wadaiwa sugu

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

KATIKA kinachoonekana kuwajali wananchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi ya shilingi Bilioni 21.3 kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza katika eneo la Buswelu Manispaa ya Ilemela Mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango mkoani humo leo Aprili 12, 2023.

Kufuatia msamaha huo, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 31.5 kama deni la msingi la msamaha wa riba uliotolewa na Rais.

Awali Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 31, 2022 kabla ya kuongeza muda ambapo sasa msamaha huo unaishia Aprili 30, 2023.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza katika eneo la Buswelu Ilemela mkoa wa Mwanza kumsikiliiza Makamu wa Rais, Dkt. Philio Mpango wakati wa ziara yake mkoani Mwanza leo.

‘’Nimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuridhia msamaha wa riba ya shilingi bilioni 21.3 ambapo wamiliki waliosamehewa wanaendelea na maisha yao na hizo fedha zitawasaidia kwa shughuli nyingine kwa hiyo wamelipa deni la msingi na ile riba wamesamehewa,’’amesema Dkt.Mabula.

Hayo yamebainishwa tarehe leo Aprili 12, 2023 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango mkoani Mwanza aliposimama kwa muda kata ya Buswelu manispaa ya Ilemela.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akizungmza na wananchi wa Buswelu mkoani Mwanza wakati wa ziara yake leo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, hadi kufikia tarehe 12 April 2023 jumla ya wamiliki wa ardhi 8,726 wamenufaika na msamaha huo huku akianisha mkoa wa Mwanza kuwa na idadi kubwa ya watu waliotumia fursa ya msamaha huo.

Aidha, Dkt. Mabula amesema wizara yake kwa sasa inakwenda kufungua mifumo yote aliyoieleza kuwa haikuwa rafiki kwa Tanzania ambapo tayari ramani za ardhi pamoja na zile za mipango miji zimebadilishwa kwa asilimia mia moja kutoka analogia kwenda digitali.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Naibu Waziri TAMISEMI Deo Ndejembi katika eneo la Buswelu wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango mkoani humo leo. Kulia ni Waziri wa Maji Jumaa Aweso.

Pia alieleza kuwa, wizara yake imeajiri kwa muda vijana wapatao 26 kwa lengo la kubadilisha mifumo itakayomuwezesha kila mtanzania kupata taarifa zake za ardhi hususan zile za kodi ya pango la ardhi kupitia simu yake ya mkononi ili kuwaepusha wananchi kufuatilia madeni yao wizarani ama ofisi za ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mpaka kufikia tarehe 12 Aprili 2023 mikoa 12 taarifa zake zimeingizwa katika mfumo ambapo wamiliki wake wataanza kupata bili zao kupitia simu ya kiganjani.
Baadhi ya Wakazi wa Buswelu Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza wakiuliza maswali wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango leo. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Vile vile, Dkt. Mabula alimshukuru Rais Samia kwa kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi huku akianisha manispaa ya Ilemela kuwa moja ya halmashauri zilizonufaika na fedha hizo iliyopatiwa jumla ya shilingi bilioni 3.589 ambapo viwanja vimepimwa na wananchi wameanza kununua kwa uwazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news