SERIKALI IMEANZA KUFANYIA KAZI TAARIFA YA CAG -WAZIRI MKUU

NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeanza kuifanyia kazi taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka baada ya kuwasilishwa rasmi Bungeni Aprili 6, mwaka huu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mawaziri Jenista Mhagama , Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) wa pili kulia wakati Bunge lilipokuwa katika maandalizi ya kuwa Kamati ya Matumizi baada ya Waziri Mkuu kutoa maelezo kuhusu hoja mbalimbali za wabunge wakati alipohitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka 2023/2024. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Tarehe 6 Aprili 2023, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliwasilishwa hapa Bungeni ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kikatiba linaloielekeza Serikali kuwasilisha Bungeni taarifa hiyo ndani ya siku saba za kazi kuanzia siku ya kikao cha kwanza cha Bunge tangu ilipowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais. Nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa Bungeni, tayari Serikali kwa upande wake imeanza kuifanyia kazi mara moja,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Aprili 13, 2023 wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa anatambua hisia za Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu ubadhirifu wa mali na fedha za umma uliobainishwa kwenye taarifa hiyo. “Sote tulishuhudia namna Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoonesha kutoridhishwa na ubadhirifu uliobainishwa katika taarifa hiyo.”
Amelieleza Bunge kuwa miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha Maafisa Masuuli wote wanaandaa majibu ya hoja, kama inavyoelekezwa katika sheria na kanuni za ukaguzi wa umma.

“Nitumie fursa hii, kuwakumbusha Maafisa Masuuli wote wazingatie maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha wanapitia kwa kina taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kujibu na kuchukua hatua za haraka juu ya hoja zote zilizoibuliwa kwenye maeneo yao,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali, taarifa ya kina kwenye maeneo yaliyobainishwa katika ripoti ya CAG, itawasilishwa Bungeni kwa kuzingatia kanuni husika.

“Nilihakikishie Bunge na wananchi kuwa kwa kuzingatia msimamo wa Mheshimiwa Rais, Serikali ya awamu ya sita haitafumbia macho matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kuwa hatua zinazochukuliwa na zitakazochukuliwa zitakuwa endelevu.”

Bunge limeidhinisha bajeti ya sh. 339,361,007,000 ambapo sh. 173,733,110,000 ni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake na sh. 165,627,897,000 ni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.

Akiwasilisha makadirio na matumizi ya ofisi yake Aprili 5, mwaka huu, Waziri Mkuu aliliomba Bunge liiidhinishe sh. 173,733,110,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 121,364,753,320/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 52,368,356,680/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.

Vilevile, aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 165,627,897,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 160,458,877,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 5,169,020,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news