SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-17

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... walipokamilisha kazi yao walirudi kambini kwao katika umbo la bundi. Walitoa maelezo kwa kina juu ya kazi waliyoifanya kwa mkuu wao, hata hivyo walielezea kazi ya ziada waliyoifanya kule kanisani.

Endelea

Ilikuwa ni asubuhi yenye utulivu, kijiupepo mwanana kilikuwa kikivuma toka Mashariki kuelekea Magharibi. Mawingu yalikuwa yamelimeza jua, hivyo kuleta hali fulani ya baridi. Kelele za shamrashamra za ndoa iliyokuwa ikitarajiwa kufungwa asubuhi hiyo ziliendelea kusikika.

Nyimbo za wasanii maarufu wa kisukuma zilitawala kwenye spika kubwa nyumbani hapo. Nyimbo za wasanii kama Ngelela,Budagala na Ng'wanakang'wa zilisikika mara kwa mara.

Vifijo, mbija na vigelegele pia vilisikika toka kwa watu waliofika harusini hapo, kila mmoja alikuwa kavalia nguo za bei mbaya, wanawake walijikwatua kwa vipodozi vya aina kwa aina huku utuli na marashi yakihanikiza maungoni mwao. Wapo waliojipaka wanja mchomoko, hina, Angle face, lipshine huku wengine wakipaka poda, nyusoni mwao.

Wazee maarufu waliketi kitako chini ya mti wa muembe mkubwa nyumbani hapo, waliketi kwa mtindo wa duara huku katikati wakiwa wameweka madebe ya pombe. Walikuwa wakijipongeza huku wakiendelea kuimba kwa nyimbo mbalimbali za kabila lao la kisukuma.

Kwa upande wa mtoto THE BOMBOM usiku wa kuamkia siku hiyo hakurudi nyumbani, alibaki kambini akiwa kategeshea kuona matokeo ya kazi yake. Kazi aliyoifanya jana usiku akishirikiana na wale wachawi watatu.

Ilipofika mida ya saa mbili na ushee walielekea barabarani akiwa na wenzie, lengo lao ilikuwa ni kumtegeshea madawa mengine Padri Samson Mcjohn atakapopita na gari lake.

Walikwenda mapema sana ili kumwahi zaidi, hakukuwa na njia yeyote ambayo angeweza kupita kuelekea kanisani kwake. Ingawa ilikuwa ni asubuhi, wachawi hao waliingia kazini pasipo uoga wa aina yeyote.

Kulingana na nguvu ya madawa yao hawakuogopa kitu, hakuna mtu ambaye angeliweza kuwaona kwa macho ya nyama.

Wakiwa kando ya barabara hiyo wakimsubiria Padri huyo, mara mchawi mkuu alimuagiza kifaa kidogo kiitwacho mbushi mtoto THE BOMBOM kule kambini, mtoto huyo aliondoka haraka kufuata alichotumwa.

Alitumia dakika chache sana kwenda na kurudi, alipofika eneo husika aliwakuta wachawi wakiendelea kumsubiri Padri huyo.

Wakati akirejea toka kambini alikotumwa, kabla ya kufika walipokuwa wenzake alifanikiwa kuiona ile gari ya Padri ikipita barabarani hapo. Cha ajabu wachawi wenzake walikuwa kwenye soga tu wala hawakujishughulisha nayo mpaka ikapita.

Alipofika aliwauliza juu ya gari hiyo wakamuona kama kachanganyikiwa, walikataa katakata kuwa hakuna gari iliyopita eneo hilo.

Mtoto huyo alichukua kiganja chake cha mkono wa kushoto, alikipunga hewani mara saba huku akizungumza kitu. Ghafla macho yao yalifunguka, kila mmoja aliweza kuliona gari la Padri huyo kwa mbali likiwa limeshapita.

Walibaki wakijilaumu kuzidiwa unjanja na Padri huyo, hawakuamini alichowafanyia mzungu huyo. Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kwa uhalisia Padri huyo alikuwa mchawi mkubwa, kwa kuwa alikuwa akitambua vita iliyokuwa mbele yake aliamu kujizindika kila kitu. Alijizindika mwili wake, usafiri aliokuwa akiutumia yaani gari, mavazi na vitu vingine vyote vikivyomzunguka.

Nguvu za kichawi alizokuwa nazo zilikuwa kubwa, japo muda wote alimhofia mtoto THE BOMBOM ambaye alikuwa na nguvu zaidi yake.

Kwa kulitambua hilo kupitia zindiko la gari lake, ndilo lililomshawishi mchawi mkuu kumuondoa mtoto huyo eneo hilo kwa kumtuma, hii ingerahisisha kwa Padri huyo kupita barabarani hapo pasipo kuonekana kwa wachawi waliosalia.

Jambo hilo lilifanikiwa kwa kiwango cha juu, Padri alipita eneo hilo huku ndani ya gari akiwa na wazungu wengine watatu pamoja na watumikiaji wawili.

Kitendo hicho kilikuwa kimewadhalilisha kwa kiwango cha juu, ni aibu! aibu kabisa! tena aibu kubwa! walijiona kuwa uchi hawakuamini macho yao kwa kile alichowafanyia Padri huyo.

Hapa ndipo walipoongeza imani za nguvu zilizokuwa ndani ya mtoto huyo mdogo, kama wao wameshindwa kuliona gari hilo iweje mtoto huyo ameweza kuliona kilahisi?.

Mtoto huyo aliwatuliza wachawi wenzake, kisha akawapa mpango mwingine wa kumnasa Padri huyo. Walitamani wamtie mikononi mwao ili wamshikishe adabu, walitaka kumdhihirishia kuwa Afrika siyo mahali pa kuchezea.

Mtoto huyo aliwashauri wachawi wenzake kurudi kambini ili wakajipange zaidi, aliwasisitiza kutokata tamaa huku akiwaaminisha kuwa kisasi kilikuwa palepale. Wachawi wote walirudi kambini japo nyoyoni walikuwa na fadhaiko kuu.

Baada ya kufika kambini walipanga mipango mbalimbali, hata hivyo walimruhusu mtoto THE BOMBOM awaelezee njia bora za kufanikisha kumnasa hasimu wao.

Mtoto huyo aliwaeleza kuwa njia rahisi ya kumkamata Padri huyo ilikuwa ni kuingiza madawa kwenye usafiri wake, madawa hayo ambayo yanaweza kusababisha ajari pindi gari litakapokuwa likisafiri.

Hakuna mchawi aliyepinga hilo, wote walikubaliana hivyo walianza kufikiria namna bora ya kuingiza madawa hayo. Jambo hilo liliwaumiza vichwa, walikuwa wakifahamu namna ilivyovigumu kulisogelea gari hilo kulingana na zindiko lake.

Wakati huo mtoto THE BOMBOM alikuwa akisikiliza mpango wa kila mmoja. Mipango yote ilionekana kugonga mwamba, hatimaye walimpa nafasi mtoto huyo awaelezee mpango wake.

Khoo! Kho! Khooooo! Alikohoa kusafisha koo lake kisha akaanza kuzungumza " Ndugu zangu kwa upande wangu nimegundua ni rahisi sana kuingiza madawa ndani gari la Padri huyo.

Njia rahisi ni kutumia fedha yaani sadaka" alipofika hapo alinyamaza kidogo huku akiwapima kama wanamuelewa alichokuwa akizungumza.

Kiumri alikuwa mdogo, lakini kiufahamu alikuwa ni zaidi ya mtu mzima, mambo yaliyowashinda kwa muda mrefu hatimaye yanapatiwa ufumbuzi na mtoto huyo.

Waliongeza imani yao juu ya mtoto huyo, waliamini kuwa ndiye atakayewavusha hakika ndiye alikuwa nabii aliyetabiriwa miaka mingi iliyopita.

Alipobaini kuwa kila mmoja alikuwa akimsikiliza kwa makini, aliendelea kuwafafanulia mpango huo. "Ndugu zangu mnakumbuka usiku wa kuamkia leo tumemuua yule kijana mtoto wa katikista? Jamii yote ya kijiji chetu haijalibaini hilo kwa kuwa tumempa uhai mfupi, tumetegeshea akadondoke na kufa kifo batili akiwa kanisani kifo hicho hakitazua mjadala ndani ya jamii.

Ndugu zangu jana baada ya kumuua kijana huyo, nilimpaka dawa pia za kuzuia Padri kutoiona misumari hiyo tuliyoigongelezea kichwani mwake. Lakini pia dawa hiyo ina nguvu ya kumdhuru Padri endapo atamgusa bwana harusi huyo.

Kwa kuwa Padri huyo ni mchawi mkuu, endapo tutamkosa huko pia niliweka madawa kwenye ekaristi ambayo ni lazima anase. Dawa hizo tulizielekeza kumdhuru muhusika tu yaani Padri, kama mtego huu akiukwepa tutamnasa kwenye sadaka.

Wachawi wote walikuwa kimya wakisikiliza mipango safi ya mtoto huyo juu ya kumnasa hasimu wao, vita yao dhidi ya Padri huyo ilikuwa ni ya muda mrefu hakuna aliyefanikiwa kumzidi mwenzie baina yao. Mtoto huyo aliendelea, "tunayo dawa ya makonza na mijolambogo, nadhani mnafahamu matumizi yake.

Kwa kuwa dawa hizi hazina madhara zikiwa peke yake, basi tunaweza kuzipaka kwenye sadaka kisha tutampa Padri huyo.

Kwa kuwa kutakuwa na ibada ama ya harusi au kifo cha kijana tuliyemuua lazima kutakuwa na sadaka, kumbukeni sadaka huwa zinawekwa kwenye chombo maalumu na kupelekwa parokiani.

Tutakuwa tumefanikiwa jaribio letu la kwanza la kuingiza dawa zetu ndani ya gari lake, hakutakuwa na shida na ni ngumu kwa upande wake kushitukia mchezo huu kwa kuwa dawa hizi zote huwa hadhina madhara zikiwa pekee.

Sehemu ya pili ya mpango wetu ni hii, tutachukua dawa ya lusona,nyondwa na mkonjomale tuakwenda kuzimwaga kwenye makutano ya barabara ya Kisesa,Ihushi na ile ya kuelekea Nyanguge maeneo ya Isangejo.

Kwa kuwa ni lazima arudi parokiani kwa kutumia barabara hiyo, atakapofika maeneo hayo dawa zilizoko kwenye sadaka ndani ya gari na zilizoko nje zitavutana kwa nguvu na kutengeneza mlipuko mkubwa. Ninaamini tutakuwa tumetengeneza ajali ambayo hakuna mtu atakayepona ndani ya gari hiyo.

Wakati wa ajali hiyo tutakuwa tumejificha eneo tukiwasubiria, pindi ajali itakapotokea tutawawahi na kuwamalizia au kumchukua Padri kwa ajili ya mambo mengine.

Kukalipuka shangwe za hali ya juu kambini hapo, kila mchawi alitamani kumbeba juu mtoto THE BOMBOM kwa mipango mizuri aliyoitoa.

Kila mchawi alikuwa na furaha juu ya mipango hiyo, walibaki wakimshangaa mtoto huyo kwa kuwa na uwezo wa hali ya juu.

Hakuna mchawi wa aina yeyote kambini hapo aliyekuwa na akifikiria mtego huo, hata hivyo kila mmoja alipiga saluti akimpongeza mtoto huyo ambaye alikuwa ni nabii kwa jamii yao.

Ndugu msomaji mambo yametaradadi, mipango ya kumnasa Padri imesukwa vyema na mtoto THE BOMBOM. Unadhani nini kitampata Padri huyo? Hebu ungana nami sehemu inayofuata.

WAYEGA ?

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news