Polisi wataja chanzo cha ajali iliyomjeruhi Naibu Waziri

NA GODFREY NNKO

JESHI la Polisi nchini limewataka wananchi kupuuza uzushi uliozushwa katika mitandao ya kijamii kwamba,katika ajali iliyohusisha gari namba T454 DWV aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikiendeshwa na Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Dkt.Festo Dugange alikuwepo mwanamke ambaye hakufahamika na kwamba alifariki katika jali hiyo.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa Aprili 29, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Martin Otieno ikifafanua kuhusu ajali hiyo ambayo ilitokea Aprili 26, mwaka huu huko jijini Dodoma.

"Mnamo Aprili 26, 2023 katika barabara ya Iyumbu maeneo ya St.Peter Clecer wilaya na Jiji la Dodoma kulitokea ajali iliyohusisha gari namba T454 DWV aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikiendeshwa na Dkt.Festo Dugange, Mbunge na Naibu Waziri wa TAMISEMI.

"Katika ajali hiyo Dkt.Festo Degange alikuwa peke yake na yeye ndiye alikuwa akiendesha gari hilo,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo ya Kamanda Otieno.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, ajali hiyo ilitokea wakati Mheshimiwa Dkt.Dugange akijaribu kumkwepa bodaboda aliyevuka barabara ghafla bila kuchukua tahadhari. "Kitendo ambacho kilipelekea gari namba T 454 DWV kugonga kingo ya barabara na kupinduka.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip I. Mpango akizungumza na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange tarehe 29 Aprili, 2023 wakati alipofika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kumjulia hali baada ya kupata ajali ya gari. Dkt. Dugange alipata ajali usiku wa tarehe 26 Aprili 2023 wakati akiendesha gari yake binafsi jijini Dodoma ambapo kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

"Katika ajali hiyo,dereva wa gari hiyo alivunjika kidole gumba cha mkono wa kulia na kupata majeraha katika mkono huo.

"Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa akiendelea kupatiwa matibabu na afya yake inaendelea kuimarika,"imefafanua kwa kina sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa, "kumekuwa na taarifa za uzushi na upotoshaji katika mitandao ya kijamii kwamba katika ajali hiyo kulikuwa na mwanamke ambaye majina yake hayafahamiki na kwamba alifariki katika ajali hiyo na pia kudai kuwamba, ajali hiyo ilihusisha gari ambalo ni mali ya Serikali.

"Taarifa hizo zipuuzwe kwani, ni za uongo na upotoshaji, gari lililohusika katika ajali hiyo ni mali ya Dkt.Festo Dugange na alikuwa peke yake katika gari hilo na yeye ndiye alikuwa dereva wa gari hilo.

"Nipende kutoa rai kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa za uongo na kuzua taharuki kwa watu bila kufanyia utafiti taarifa hizo kabla ya kusambaza katika mitandao ya kijamii.

"Jeshi la Polisi liko macho na makini kufuatilia na kutoa ufafanuzi wa taarifa zozote, hivyo wananchi msisite kufika kwetu na kupata ufafanuzi wa taarifa zozote mnazotilia mashaka,"amefafanua Kamanda Otieno. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news