Vijiji 32 vyapata maji ya bomba Musoma Vijijini, Prof.Muhongo ashukuru

NA FRESHA KINASA

JUHUDI za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi zimeendelea kushika kasi.

Ambapo vijiji 32 katika Jimbo la Musoma Vijijini tayari vimepata maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria huku vingine vikiendelea kufikiwa na huduma hiyo muhimu.

Akizungumzia hatua hiyo njema Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo amesema, hatua hiyo ni hatua kubwa na njema iliyofanywa na serikali katika kuwafikishia huduma wananchi ambapo kwa sasa wananufaika na uongozi makini wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan unaojali mahitaji ya wananchi wake.

Amebainisha kwamba katika kipindi kifupi kazi kubwa imefanyika kuwafikishia wananchi maji hasa kwenye maeneo ambayo yalikuwa hayana maji jimboni humo na hivyo wananchi kuwapa neema kwa kuwatua ndoo kichwani kina mama ambayo ndio dhamira thabiti ya serikali.

Ameongeza kuwa, vijiji vyote 68 vilivyopo Jimbo la Musoma Vijijini vina miradi ya maji inayoendelea ikiwemo ya visima na kutoka Ziwa Victoria.

Amesema, vijiji 15 vimepatiwa fedha za miradi ya maji na kazi inaendelea kwa kasi ili kuweza kuwafikishia wananchi maji kwenye maeneo yao.

Mbunge huyo amedai kuwa vijiji 12 vinavyosimamiwa na RUWASA na saba vilivyo chini ya MUWASA vinakamilishiwa usanifu na vipo kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024.

"Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia miradi mingi ya maji ambayo inakwenda kwa kasi.

" Usimamizi wa RUWASA na MUWASA ni mzuri na miradi yetu yote inakwenda vizuri ya maji kutoka Ziwa Victoria na ile ya visima,"amesema Prof.Muhongo.

Amesema, maji ni uchumi na maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kulinda na kutunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Neema Athanas ambaye ni Mkazi wa Nyakatende katika Jimbo la Musoma Vijijini amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt.Samia kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ambapo amesema hatua hiyo inachagiza maendeleo kwani badala ya muda mwingi kutumika kutafuta maji, muda huo utatumika kufanya kazi za uzalishaji.

"Mbunge Prof. Muhongo anafuatilia miradi mingi ya Maendeleo jimboni mwetu na pia Rais anatoa fedha za miradi kwa hiyo Serikali kwa ujumla inatujali Wananchi Mimi nimshukuru Rais kuzidi kutukumbuka kina mama kututua ndoo kichwani Mungu azidi kumbariki na pia Mbunge kwa juhudi za kufuatilia miradi kwa ukaribu kwa ajili ya wana-Musoma Vijijini,"amesema Jesca Bwire.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news