Wasanii watano washikiliwa kwa kuharibu ofisi ya Serikali jijini Mwanza

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata watu watano kwa tuhuma za kosa la kuharibu mali na kufanya mkusanyiko usio halali katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kishiri ‘A’ Wilaya ya Nyamagana.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Wilbrod Mutafungwa ikifafanua kuhusu tukio hilo.

Kamanda Mutafungwa amesema, Aprili 27, mwaka huu majira ya saa 20:00 huko katika kiwanja cha Ofisi ya Serikali za Mtaa wa Kishiri ‘A’, Kata ya Kishiri, Wilaya ya Nyamagana, msanii wa nyimbo za asili aitwaye Mateso Julius, miaka 27 akiwa na wenzake wa wanne waliandaa tamasha la muziki katika kiwanja hicho bila kuwa na kibali cha kufanya tamasha hilo.

Baada ya kusikia kelele za muziki huo, Afisa Mtendaji wa kata hiyo, John Mwakalasya katika eneo hilo na kuwaomba kibali cha kufanya tamasha hilo ambapo alibaini kuwa wanamuziki hao hawakuwa na kibali hivyo, aliwataka waache kuandaa tamasha hilo hadi watakapopata kibali.

Kamanda huyo amefafanua kuwa,wasanii hao walikaidi maelekezo hayo na kuendelea kuandaa tamasha huku wakipiga muziki kwa sauti ya juu wakiwa na spika zilizokuwa ndani ya gari lao aina ya Canter namba T. 235 DFK.

Amesema, Afisa Mtendaji aliwasisitiza tena kuacha mara moja kufanya tamasha hilo na kuondoka eneo hilo ndipo wasanii hao walianza vurugu za kurusha mawe kwenye ofisi ya mtendaji kata ambapo walivunja vioo vya madirisha ya ofisi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kamanda, taarifa hizo ziliripotiwa Kituo cha Polisi Nyakato kwa haraka na askari walifika eneo la tukio na kuwaamuru wanamuziki hao kuacha kuendesha tamasha hilo bila kibali ambapo walikaidi, ndipo askari walitawanya mkusanyiko huo usio wa halali na kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni:-

1. Mateso Julius (27)
2. Samson Sylvester (30)
3. Magereza Lazaro (30)
4. Lucas Samson (21)
5. Emmanuel Ntambi (30)

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa rai kwa wananchi kufuata sheria na taratibu za kufanya tamasha na kupiga muziki katika maeneo yenye makazi ya watu. Pia, linawasihi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ili ziweze kufanyiwa kazi,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news