Bilionea Microsoft kufanya “Royal Tour” Tanzania

NA MWANDISHI WETU

MMOJA wa wanahisa wa kampuni mashuhuri duniani ya Microsoft na akihudumu kwa miaka 14 kama Mtendaji Mkuu wa Masuala ya Teknolojia, Dkt. Nathan Myhrvold ameeleza kuvutiwa na hali ya utalii nchini Tanzania ikiwemo juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuitangaza nchi kupitia filamu ya “Tanzania; The Royal Tour.” 
Dkt. Nathan ameyasema hayo jana Mei 9, 2023 alipokutana katika ofisi za kampuni yake ya “Intellectual Ventures” mjini hapa na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi.

“Ninavutiwa sana na vivutio vya utalii vya Tanzania na wale waongoza utalii wazuri wanaoijua kazi yao hasa nimeshafika Serengeti na Ngorongoro na napongeza juhudi za Rais wenu kuutangaza utalii kwa sababu naamini hicho ndicho nilichoona kwa miaka mingi kilihitajika kufanywa ikilinganishwa na nchi nyingine,” alisema.
Kwa upande wake Dkt. Abbasi aliyeambatana na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Damasi Mfugale, alimkaribisha tena Tanzania bilionea huyo ambaye pamoja na Microsoft na kampuni ya Intellectual Venture ambayo ni Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu, pia wamewekeza pamoja na Bill Gates katika kampuni nyingine kubwa ya utafiti wa masuala ya Umeme salama ya TerraPower. 
“Ili kuipa fursa Tanzania kunufaika zaidi na utalii wake, Rais wetu Mhe Samia Suluhu Hassan kwa sasa anawekeza nguvu kubwa katika kuitangaza Tanzania na unaweza kuona alivyotoka na kwenda maeneo mbalimbali kupitia filamu ya Royal Tour iliyoko katika mitandao ya Amazon na Apple TV,” alisema Dkt. Abbasi akimuelezea Bilionea huyo na mmoja wa wagunduzi wakubwa kwa sasa duniani.
“Nilikuwa na maandalizi ya kuja tena Tanzania, sasa mmenivutia zaidi nitakuja Tanzania Juni mwaka huu,” alisema Dkt. Nathan akitaja hifadhi mbili kubwa anazopanga kuzitembelea hasa pia akipenda kuendeleza tafiti zake binafsi kuhusu vyakula vya asili na wanyama jamii ya paka wakubwa.
Pamoja na utajiri wake unaofikia Dola za Marekani Bilioni 700, kuwa mmoja wa wanasayansi na wagunduzi wakubwa wa nyakati hizi na mmoja wa wagunduzi wa programu ya “microsoft windows,” Dkt. Nathan pia ni mwandishi mwenza na Bill Gates wa kitabu mashuhuri duniani kiitwacho “The Road Ahead.” 

Wakiwa kwenye taasisi ya Intelectual Ventures, pamoja na mambo mengine, ujumbe huo wa Tanzania ulijionea maabara mbalimbali za utafiti wa vifaa na tiba za afya na jinsi kampuni hiyo pia inavyoendeleza utafiti katika masuala ya vyakula na kamera za upigaji picha maeneo ya kitalii na anga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news