CCM yaitaka Serikali kutafuta kiini mgogoro wa wafanyabiashara Kariakoo

NA DIRAMAKINI

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeitaka Serikali kutafuta kiini cha mgogoro wa wafanyabiashara Kariakoo jijini Dar es Salaam na kuhakikisha inaupatia ufumbuzi.

Kamati hiyo imetoa maelekezo hayo katika kikao chake maalum kilichoongozwa leo Mei 21, 2023 na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea na kujadili taarifa kuhusu mgogoro wa wafanyabiashara wa soko hilo la Kimataifa.

“Kamati Kuu baada ya kujadili imeielekeza Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa masuala yaliyoibuliwa na kulalamikiwa na wafanyabiashara wa Kariakoo ili kutafuta kiini cha tatizo halisi na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu,”imesema taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema.

Pia, Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuhakikisha inatengeneza utaratibu wa kutatua changamoto mapema kabla hazijaleta madhara katika jamii kama ilivyokuwa katika mgogoro wa soko la Kariakoo.

Kamati Kuu imetoa maelekezo hayo kwa Serikali ikiwa ni siku nne zipite tangu wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamalize mgomo wao ambao ulifanyika kwa siku tatu mfululizo kwa kufunga maduka yao kushinikiza kutolewa kwa kodi ya stoo na kukomeshwa kwa kile walichokiita kamatakamata inayofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Aidha, mgomo huo ulitamatika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya vikao viwili na wafanyabiashara hao huku kikao cha kwanza kilichofanyika Mei 15, 2023 kisifue dafu na baadhi ya wafanyabiashara waliendelea na mgomo hivyo kulazimika tena Mei 17, 2023 kufanya kikao kingine cha wazi katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Katika kikao cha pili kilichohudhuriwa na mamia ya wafanyabiashara wa soko hilo kilifanikisha kumaliza mgogoro huo baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Nchemba na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt.Ashatu Kijaji kuwasikiliza wafanyabiashara hao na baadaye kuunda kamati ya watu 14 kushughulikia matatizo hayo ikiwahusisha wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.

Wakati huo huo Kamati Kuu imempongeza Rais Dkt.Samia kwa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya na kukamilisha ujenzi wa Ikulu mpya ya Chamwino iliyozinduliwa rasmi Mei 20, 2023 mkoani Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news