Hospitali ya Mirembe kubadilishwa jina kuwa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali inatarajia kubadilisha jina la Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na kuitwa National Istititue for Mental Health (Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili).
Mheshimiwa Waziri Ummy ameyasema hayo Mei 9,2023 kwenye semina maalum iliyoandaliwa kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kupata elimu ya masuala ya afya ya akili, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD). 
“Tunakwenda kubadili jina la Hospitali ya Mirembe ili kujenga taswira mpya ndani ya jamii kwenye huduma zinaotolewa pale, mtu anaweza kwenda pale kutibiwa hata malaria, lakini jamii inamuita ‘chizi’. Tunataka Mirembe iitwe National Istititue for Mental Health,”amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Mheshimiwa Waziri Ummy amefafanua kuwa, “Tunataka Hospitali ya Mirembe ifanye kampeni za hamasa na kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya ya akili, matibabu, tafiti mbalimbali za masuala ya afya ya akili pamoja na kufanya mafunzo,”amesema Waziri Ummy.

Pia amesema, wizara itaendelea kusimamia huduma za matibabu ya afya ya akili nchini kwa kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma hizo, huku akiwataka wananchi kutoogopa kujitokeza kupata huduma hizo kwa wataalamu.
“Usione aibu kulia, kulia ni tiba ya afya ya akili, kwa changamoto ambazo tunapitia ni dhahiri kuwa wananchi wanapata sonona, wanakosa usingizi hizo zote ni changamoto na dalili za afya ya akili,”amefafanua Mheshimiwa Waziri Ummy.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Mhe.Stanslaus Nyongo akiwawakilisha wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema,ni vizuri Wizara ya Afya ikawa na kampeni maalumu ya kutoa elimu ya afya ya akili ili watu wanapotaka kupata huduma za afya ya akili wajue pa kwenda.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dkt.Omary Ubuguyu amesema kuwa, tatizo la afya ya akili ni kubwa duniani na huathiri asilimia 13 ya watu wote na kwa Tanzania tatizo hilo ni kati asilimia 4.2 hadi 6 zikiwaathiri zaidi watu wenye umri wa miaka 15 hadi 29.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news