Wizara yatoa maagizo kuhusu mwanamke aliyechomwa sindano katika duka la dawa na kumsababishia madhara

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Afya imeelezea kupokea kwa masikitiko kuhusu taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia Mei 7,2023 kuhusiana na Bi.Esther Mkombozi mkazi wa Mtaa wa Kimandolu mkoani Arusha ambaye ameeleza kuwa, alichomwa sindano katika duka la dawa na kumsababishia madhara katika mkono wake.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 9,2023 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Bw.Aminiel Buberwa Aligaesha.

"Tunapenda kuufahamisha umma kuwa, ni kosa kisheria kwa duka lolote la dawa nchini kutoa huduma za kitabibu ikiwa ni pamoja na kuchoma sindano, kufanya tohara au vipimo vya kimaabara.

"Kutokana na hilo, Wizara imeelekeza Baraza la Famasia (PC) na Bodi ya Hospitali Binafsi (PHAB) kufuatilia suala hili mara moja ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wote watakaobainika kukiuka sheria, kanuni, miongozo na taratibu za usimamizi na udhibiti wa utoaji wa huduma za afya nchini.

"Tunampa pole, Bi.Esther kutokana na madhara aliyoyapata. Tunawaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu ambapo suala hili linafanyiwa kazi.

"Wizara yya Afya inatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapata huduma za afya katika maeneo stahikiu ikiwemo hospitali, vituo vya afya na zahanati ili kuepuka madhara na athari mbalimbali zinazoweza kuwapata ikiwa watakwenda sehemu zisizo rasmi,"imefafanua kwa kina sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news