HUPUUZWA MPUUZI

NA LWAGA MWAMBANDE

MEI 30, 2023 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameonesha kukerwa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa ambao mara nyingi badala ya kujenga hoja zenye manufaa kwa ustawi bora wa wananchi na nchi, wamekuwa wakiibua propaganda ambazo hazina umuhimu wowote na afya kwa jamii.

Rais Dkt.Mwinyi kupitia mkutano wake wa kawaida wa kila mwezi na waandishi wa habari ambao umefanyika Ikulu jijini Zanzibar anasema,mara zote mambo ya kipuuzi hayapaswi hata kusikilizwa, achilia mbali kujibiwa.

"Labda na mimi nichukue fursa hii, kama nilivyosema siku za nyuma, kwamba upotoshaji lazima tuutolee ufafanuzi ili watu wasiendelee kupotoshwa, lakini masuala ambayo mimi ninayaita ya kipuuzi, upuuzi haujibiwi, unapuuzwa.

"Kwa hiyo mtanisamee yale ambayo mimi ninayahesabu ya kipuuzi, kwa sababu hayapaswi hata kusikilizwa, achilia mbali kujibiwa.

"Kuhusu ili la kwamba CCM haijawahi kushinda, ndiyo yale niliyoyasema, upuuzi haujibiwi, upuuzwa ili siwezi kulijibu, nani asiyejua mfumo wa uchaguzi wa nchi yetu, maana wengine wanajibu toka kwenye kura za maoni ndani ya CCM ah! kampewa tu na Mwenyekiti...

"Jamani kuna mwaka ambao ulikuwa wazi katika uchaguzi kuliko mwaka huu wa uchaguzi, mwaka huu wa uchaguzi kura zilipigwa hadharani na zimehesabiwa hadharani, imewahi kutokea ile?.

"Sasa mtu akianza kuzungumza maneno hayo ya ovyo unamjibu au unampuuza? Mimi kwa ili naomba nimpuuze kwa sababu halipaswi kusikilizwa achilia mbali kujibiwa," amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi katika mkutano huo na vyombo mbalimbali vya habari, ambapo alitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yaliyoulizwa katika mkutano huo,"alisisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,mtu anayesema hovyo yafaa kuendelea kupuuzwa zaidi kama hatakuwa tayari kujishusha na kujifunza. Endelea;

1.Hupuuzwa upuuzi, haujibiwi kaabiwa,
Ukiwa ni kiongozi, hilo wapaswa elewa,
Kwanza ni kukosa kazi, ndivyo unavyoambiwa,
Tukitangaziwa kafa, linalobaki kaburi.

2.Kama mtu amekufa, tayari tumeambiwa,
Ndiyo hivyo amekufa, tunapaswa kuelewa,
Vinginevyo hizo nyufa, ndio zinapaliliwa,
Tukitangaziwa kafa, linalobaki kaburi.

3.Na mwingine yuko hai, twasikia twaambiwa,
Hapo nenda kunywa chai, kwa unayefurahiwa,
Kama waweza kudai, wako wanashitakiwa,
Tukitangaziwa kafa, linalobaki kaburi.

4.Maiti kuifukua, kifo ukakielewa,
Au kama waagua, hadi ukafunuliwa,
Tangazo kulitengua, pengine umeshalewa,
Tukitangaziwa kafa, linalobaki kaburi.

5.Anayesema ya hovyo, kufika ananogewa,
Hata maswali ya hivyo, mtu unayeelewa,
Wamwacha jinsi alivyo, jibu atalielewa,
Tukitangaziwa kafa, linalobaki kaburi.

6.Usiseme kipuuzi, mwisho ukazodolewa,
Ushuke toke ngazi, kama maji wamwagiwa,
Uliza yenye ujuzi, ili uweze jibiwa,
Tukitangazwa kafa, linalobaki kaburi.

7.Walishatangaza kafa, mwili ukachukuliwa,
Wanabakia malofa, kichaa kasingiziwa,
Mkizika weka dhifa, amekwishapokelewa,
Tukitangaziwa kafa, linalobaki kaburi.

8.Kupanda kwa mstari, ndivyo tunashauriwa,
Mbolea weka vizuri, mihula waielewa,
Mbona unazua shari, walovuna wachekewa,
Tukitangaziwa kafa, linalobaki kaburi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news