Malawi yaishukuru Tanzania kwa kutoa huduma za matibabu ya moyo

NA MWANDISHI MAALUM
Blantyre 

SERIKALI ya Malawi imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapeleka wataalam wa moyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa nchi hiyo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela akimpima jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – Echo) mtoto kutoka nchini Malawi wakati madaktari bingwa wa JKCI walipofanya kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya nchini Malawi, Mhe. Khumbize Chiponda alipotembelea Hospitali ya Queen Elizabeth kuangalia huduma zilizokuwa zikitolewa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo.

Mhe. Khumbize alisema Malawi na Tanzania wamekubaliana kuwa na kushirikiano katika kujengeana uwezo kwani nchi hiyo bado haijaweza kuanzisha hospitali ya moyo hivyo kupitia kambi hiyo wataenda kujitathimini uwezo wao kama wanaweza kuanzisha kituo ambacho kitakuwa kinatoa huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo nchini humo.

“Ndugu zetu watanzania wapo mbele yetu katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwasababu yatari wameshafungua Taasisi ambayo inatoa huduma za moyo na imewekeza wataalamu na vifaa vya kutosha, naamini tukiendelea kupata ujuzi kama huu nasi tutaweza kufungua Hospitali ya Moyo”, alisema Mhe. Khumbize
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazaura na mwenzake kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi wakiangalia majibu ya mgonjwa aliyefanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram - Echo) wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyofanywa na madaktari hao nchini Malawi katika Hospitali ya Queen Elizabeth. 

Mhe. Khumbize alisema matibabu ya moyo ni ya gharama, hadi sasa Malawi ina wagonjwa zaidi ya mia tano wenye gamonjwa mbalimbali ya moyo wanaosubiria kuwapeleka nje ya Malawi kwa ajili ya matibabu.

Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazaura alisema katika kambi hiyo walifanya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watu wazima na watoto ambapo kila siku watoto zaidi ya 80 wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi wa moyo na kubaini watoto wengi walikuwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo na wachache kuwa na magonjwa ya moyo waliyoyapata wakati wa ukuaji.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Georgy Longopa na mwenzake bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi Dkt. David McCalthy wakijadili matibabu anayopaswa kupewa mgonjwa mara baada ya kumfanyia uchunguzi wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.

“Kwa bahati mbaya watoto wengi wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wamekuja wakiwa na umri mkubwa ambapo ilipaswa kufanyiwa upasuaji mapema baada ya kuzaliwa lakini hawakufanyiwa kutokana na huduma hizi kutokuwepo hapa Malawi."

Dkt. Parvina alisema watoto ambao kutokana na umri wao kupita wakati wa kufanyiwa upasuaji wa moyo wameangalia matibabu wanayoendelea kuyapata na kuwashauri wataalam wa afya wanaowahudumia ni dawa gani wanapaswa kuzitumia ili waweze kuwa sawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi, Dkt. Chimota Phiri alisema kambi ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wenzeo kutoka JKCI imewapa mwanga wa kuyatambua magonjwa mbalimbali ya moyo waliyonayo wananchi wa Malawi

“Nchi yetu sasa inatakiwa kuwekeza katika taaluma ya kibingwa ya matibabu ya moyo ili wataalam wetu waweze kwenda kujifunza na kuwasaidia wananchi wetu kupata huduma hapa nchini badala ya kuanza kuhangaika kutafuta huduma za matibabu ya moyo nchi za mbali,”alisema Chimota.
Baadhi ya wananchi wa Malawi wakisubiri kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.

Lay Pastor Kachoka mwananchi wa Malawi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo amewashukuru madaktari kutoka JKCI kwa kumfanyia uchunguzi wa kina na kumshauri kuhudhuria kliniki ya matibabu ya moyo kila baada ya miezi sita.

“Sisi wananchi wa Malawi tunahitaji sana huduma hizi kuwepo hapa nchini kwetu, nawashauri wakati mwingine watakapoandaa kambi kama hii waweke maeneo tofauti tofauti ya nchi yetu ili wananchi wote waweze kufaidika na huduma hizi”, alisema Lay Postor.

Katika kambi hiyo ya matibabu ya moyo ya siku tano iliyomalizika jana nchini Malawi jumla ya watu 724 walifanyiwa uchunguzi ambapo kati yao watu wazima walikuwa 494 na watoto 230.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news