Profesa Jay afunguka kwa mara ya kwanza

NA DIRAMAKINI

MKONGWE wa Hip Hop Bongo, Profesa Jay ambaye kwa muda mrefu anaumwa,hali ya afya yake imeendelea kuimarika baada ya kurudi tena kwenye mitandao ya kijamii.

Ni baada ya ukimya uliodumu karibu mwaka mmoja na nusu wa kutokuweka chochote kwenye kurasa zake baada ya kuugua na kulazwa hospitali ambapo kwenye machapisho yake ameweka picha ya muonekano wake wa sasa.

"Salaam ndugu zangu, kwanza namshukuru sana MUNGU aliye hai kwa uponyaji na kunipa nafasi nyingine ya kuendelea kuwa hai, hali yangu ilikuwa mbaya isioelezeka, asante sana Mungu baba (nitakutukuza na kukusifu siku zote za maisha yangu),

"Pili kipekee namshukuru sana Mhe. Rais Dr. Samia Hassan Suluhu na Serikali yake kwa kunigharamia matibabu yangu yote ya Muhimbili na Nje ya Nchi, Asante sana Mama pamoja na Serikali yako yote kwani Viongozi wako wa chama na serikali walikuwa wanapishana kila siku kuja kuniona na kunifariji.

"Tatu namshukuru sana Mwenyekiti wa Chama changu cha CHADEMA Kamanda Freeman Mbowe, Wanachama na Viongozi wote waandamizi wa Chama kwa jitihada zao za kuhakikisha napata matibabu bora zaidi kwa kushirikiana na Serikali.

"Zaidi nawashukuru sana Madaktari na Manesi wote wa Muhimbili kwa kunipa matibabu ya kiwango cha juu kwa zaidi ya mwaka mzima niliolala hapo Muhimbili hasa zile siku 127 za hatari nilizokuwa nimelazwa ICU, mlijitoa kwa uwezo wenu wote kuhakikisha kuwa mnaokoa uhai wangu AHSANTENI SANA,"amefafanua Profes Jay.

Pia amewashukuru Watanzania wote waliojitolea kwa maombi na pesa ambazo zilimsaidia sana kulipia gharama za awali kabla ya Serikali kuingilia kati na kusema itagharamia kila kitu.

Watanzania mbalimbali aliowashukuru Profesa Jay ni pamoja na Malisa GJ, Iyenda,vyombo vyote vya habari na mitando ya kijamii ikwemo Clouds FM, Millard Ayo, Wasafi FM,watumishi wa Mungu kama Wachungaji, Mashekh na Mapadri, Familia yake akiwemo Mke wake, Kaka zake, Dada zake, Wadogo zake na Familia yote ya Mzee Haule.

"Kwa sasa nipo imara na ninaendelea vizuri sana Mungu ni mwema sana siku zote🙏🏻🙏🏻🙏🏻,Ahsanteni…… Joseph Haule (Prof. Jay) #MgodiUnaotembea #SeeYouSoon ❤️❤️❤️❤️."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news