Rais Dkt.Mwinyi azindua Kamati ya Maridhiano kati ya CCM na ACT Wazalendo

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi awashukuru viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo kwa kukubali kukaa pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuendeleza dhamira ya kushirikiana na kuimarisha Umoja wa Kitaifa Zanzibar. 
Ameyasema hayo leo alipozindua Kamati ya Maridhiano kati ya CCM na ACT Wazalendo Ikulu, Zanzibar. 

Aidha,Dkt.Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuridhia, kufanya vikao na viongozi wa vyama vya siasa na kusikiliza maoni yao ambayo ameendelea kuyafanyia kazi na kutekeleza kwa vitendo azma ya kuleta maridhiano ya kisiasa ikiwemo kuunda Kikosi Kazi kilichopitia ripoti ya mkutano wa Baraza la vyama vya siasa na kutoa mapendekezo.

Vilevile kwa kuimarisha uhuru wa kisiasa na kidemokrasia kwa kuruhusu tena mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Dkt.Mwinyi amesema hotuba yake aliyoitoa Mwezi Novemba Mwaka 2020 wakati anazindua Baraza la Wawakilishi kuwa dhamira yake ni kuwaunganisha wananchi wote wa Zanzibar kuwa wamoja, bila kujali rangi, asili, imani za dini au itikadi za kisiasa.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman na ujumbe wake pamoja na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Mjumbe wa kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Mhe.Hemed Suleiman Abdullah na ujumbe wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news